Air France-KLM yamtangaza Joris Holtus Meneja Mkuu Afrika Mashariki, Kusini, Nigeria na Ghana

Kampuni ya ndege ya Air France-KLM imemtangaza Joris Holtus kuwa Meneja Mkuu mpya anayesimamia shughuli za kampuni hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, pamoja na nchi za Nigeria na Ghana. Uteuzi huu unaanza kutekelezwa mara moja, ambapo Holtus anachukua nafasi ya Marius van der Ham aliyeongoza eneo hilo kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kabla ya uteuzi huu, Holtus alikuwa Makamu wa Rais wa Mipango na Maendeleo ya Mauzo katika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Amstelveen, Uholanzi na Paris – Roissy-Charles de Gaulle, ambapo aliongoza timu ya watu 100 katika kuandaa mikakati ya kimataifa ya mauzo, sera na bidhaa.

Holtus ana uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika uongozi wa juu katika mabara manne, ikiwa ni pamoja na Afrika ambako aliwahi kuwa Meneja Mkuu wa Air France-KLM nchini Afrika Kusini, akihusika na majukumu ya kibiashara, kiutendaji na kiutawala kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Tunafuraha kubwa kumkaribisha tena Joris Holtus barani Afrika katika nafasi hii muhimu ya uongozi,” alisema Hildabeta Amiani, Meneja wa Mauzo wa Air France-KLM nchini Kenya. “Uelewa wake wa kina kuhusu masoko mbalimbali, uwezo wake wa kuleta mabadiliko na mapenzi yake kwa watu vinamfanya awe chaguo sahihi kwa kuendeleza ukuaji wa kampuni katika ukanda huu unaokua kwa kasi.”

Katika nafasi yake ya awali, Holtus alisimamia mabadiliko makubwa ya muundo wa kimataifa wa mauzo kwa kutumia ubunifu wa kiteknolojia na mbinu mpya za kiutendaji ili kuongeza ufanisi wa huduma. Baadhi ya mafanikio makubwa katika taaluma yake ni pamoja na:

  • Kuzindua mpango wa Corporate Sustainable Aviation Fuel (SAF) wa Air France-KLM — wa kwanza wa aina yake katika sekta ya usafiri wa anga duniani.
  • Kuongoza mabadiliko ya kidigitali na kuboresha huduma kwa wateja kwa kiwango cha juu.
  • Kusimamia ongezeko la mapato na upanuzi wa mtandao wa safari katika Amerika ya Kusini na Karibiani akiwa kama Meneja Mkuu wa Mid-Americas & Dutch Caribbean.
  • Kuwezesha huduma bunifu kama SkyPriority na KLM’s Meet & Seat, zilizoshinda tuzo mbalimbali za kimataifa.

Joris Holtus alizaliwa katika mji wa Hertogenbosch, Uholanzi, na anashikilia Shahada ya Uzamili ya Uchumi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Vrije Universiteit Amsterdam. Anazungumza lugha ya Kiholanzi na Kiingereza kwa ufasaha, na ana uzoefu wa kikazi katika lugha ya Kijerumani na Kihispania.

“Ninaheshimika kurejea tena barani Afrika katika kipindi hiki cha mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri wa anga,” alisema Holtus. “Masoko ya Afrika Mashariki, Kusini na Magharibi yana fursa nyingi na changamoto zinazohitaji ubunifu. Natarajia kushirikiana na timu zetu pamoja na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma na kuongeza muunganisho wa safari ndani ya bara hili.”

Uteuzi wa Holtus unakuja wakati ambapo Air France-KLM inaendelea kupanua huduma zake katika ukanda wa Afrika Mashariki. Hivi karibuni, Air France imeanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, hatua inayoashiria dhamira ya kampuni hiyo kuimarisha uwepo wake kaskazini mwa Tanzania.

Kwa upande mwingine, KLM inaendelea kutoa huduma za ndege mara saba kwa wiki kuelekea Dar es Salaam kupitia Amsterdam, huku safari za Kilimanjaro zikifanyika mara tano kwa wiki na Zanzibar mara mbili kwa wiki. Hii inawapa abiria fursa zaidi za kusafiri kwa urahisi ndani na nje ya Tanzania.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *