Historia mpya inasukwa. Klabu ya Azam FC inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote leo ili kuweka rekodi ya kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup).
Azam itashuka dimbani Azam Complex, Dar es Salaam, kuikaribisha KMKM ya Zanzibar katika mchezo wa marudiano, ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata wiki iliyopita visiwani Zanzibar.
Kocha Msaidizi wa Azam, Kassim Liogope, alisema kikosi chake kimejipanga vyema kuhakikisha kinaitumia fursa hiyo kuandika historia.
“Tunafahamu tunakutana na timu ambayo tumewahi kucheza nayo, lakini huu ni mchezo tofauti na muhimu. Unakwenda kubadili historia ya klabu yetu katika ramani ya soka la Afrika,” alisema Liogope.
Liogope aliongeza kuwa kila mchezaji anafahamu uzito wa mchezo huo, akisisitiza kuwa makosa madogo yanaweza kugharimu ndoto yao ya kufuzu hatua ya makundi.
Aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia historia ikiandikwa nyumbani.
Kipa wa timu hiyo, Aishi Manula, alisema wamejipanga vyema na morali ipo juu.
“Kila mchezaji ana kiu ya kufanya vizuri. Tunajua KMKM itakuja kwa nguvu, lakini tunataka historia ibaki Azam Complex,” alisema Manula.
Kwa upande wa wapinzani wao, Kocha Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali, alisema wamejipanga kupambana licha ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani.
“Tunajua itakuwa mechi ngumu, lakini tutacheza kwa nidhamu na ubunifu. Hata kama hatutafuzu, tutatumia mchezo huu kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao,” alisema Hababuu.
Nahodha wa KMKM, Martin Londo, alisema wapo tayari kwa mapambano licha ya kutambua ubora wa wapinzani wao.
“Tunaiheshimu Azam, lakini na sisi hatuji kukata tamaa. Tunataka matokeo chanya,” alisema Londo.
Ofisa Habari wa Azam, Hasheem Ibwe, alisema mageti ya Azam Complex yatafunguliwa kuanzia saa 4:00 asubuhi, na mashabiki wataingia bure kwenye mzunguko, huku VIP A na B zikiwa kwa wageni maalum.




