Friday, March 6, 2026
spot_img
HomeHabariBalozi Kaganda, Ethiopia wajadili ushirikiano

Balozi Kaganda, Ethiopia wajadili ushirikiano


Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Zimbabwe, Rashid Mohammed Abdulwahid, ambapo wamejadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia katika nyanja mbalimbali.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kaganda aliishukuru Serikali ya Ethiopia kwa kuendelea kudumisha urafiki wa muda mrefu na Tanzania. Alieleza kuwa uhusiano huo ulianzishwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Hayati Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia.

Aidha, Balozi Kaganda aliipongeza Ethiopia kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2026. Alisema Tanzania, kama mshirika wa karibu wa Ethiopia, inawatakia wananchi wa nchi hiyo amani, umoja na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Balozi Abdulwahid alimshukuru Balozi Kaganda kwa kutenga muda wake kwa ajili ya mazungumzo hayo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha namna Tanzania na Ethiopia zinavyoendelea kuthamini na kuendeleza misingi ya kindugu iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo.

Aliongeza kuwa anatambua mchango unaotolewa na Tanzania kwa Ethiopia katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, ikiwemo kuunga mkono jitihada za nchi hiyo katika kuwania nafasi mbalimbali katika taasisi na majukwaa hayo.

Katika hatua nyingine, Balozi Kaganda alitembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Indonesia nchini Zimbabwe kwa ajili ya kutoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais Mstaafu wa Indonesia, Jenerali Mstaafu Try Sutrisno, aliyefariki dunia Machi 2, 2026.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni ishara ya mshikamano na kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Indonesia.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments