Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariBaraza la 11 la Wawakilishi kuanza kesho, Uchaguzi wa Spika kipaumbele

Baraza la 11 la Wawakilishi kuanza kesho, Uchaguzi wa Spika kipaumbele

Baraza la 11 la Wawakilishi linatarajiwa kuanza mkutano wake wa kwanza kesho, Novemba 6, 2025, ambapo shughuli kuu zitakazofanyika ni pamoja na uchaguzi wa Spika wa Baraza hilo.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, ametoa taarifa hiyo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Chukwani, Zanzibar.

Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 73(1) kinawataka wajumbe wateule wa Baraza kumchagua mjumbe mmoja miongoni mwao au mtu mwenye sifa za kuwa Mwakilishi kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Aidha, Mselem ameongeza kuwa uchaguzi wa Spika ndiyo shughuli pekee ambayo mjumbe anaweza kuifanya bila kula kiapo cha uaminifu, kwa mujibu wa kifungu cha 70 cha Katiba ya Zanzibar.

Baada ya uchaguzi huo, amesema Katibu wa Baraza atamuapisha Spika mteule, ambaye naye ataongoza kiapo cha uaminifu kwa wajumbe wote wa Baraza, kama inavyoelekezwa katika masharti ya kifungu cha 70 cha Katiba.

Mkutano huo wa kwanza unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa shughuli za Baraza la 11 la Wawakilishi, kufuatia kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika hivi karibuni.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments