Kiasi cha Sh. bilioni 12.8 kimetumika kukarabati kilomita 13.1 za barabara ya Iringa–Mtera, ambayo ni kiunganishi muhimu cha jamii, biashara na huduma za kijamii. Ukarabati huo mkubwa umelenga kuongeza usalama, ufanisi na uimara wa miundombinu hiyo muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa ya matengenezo iliyosomwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Yudas Msangi, mradi huo umehusisha matengenezo ya jumla ya kilomita 13.1 kwa gharama ya Sh. bilioni 12.8.
Taarifa hiyo iliwasilishwa mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Mussa Natty, pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA), Mhandisi Rashid Kalimbaga, wakati wa ziara yao ya kukagua utekelezaji wa kazi za matengenezo.
Mhandisi Msangi alieleza kuwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuziba mashimo, kuimarisha tabaka la juu la barabara, kuboresha mifumo ya mifereji ya maji na kuweka alama za barabarani kwa lengo la kuongeza usalama kwa watumiaji.
Alisema maboresho hayo yamechangia kupunguza gharama za uendeshaji wa magari, kupunguza muda wa safari na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Iringa na Mtera.
Zaidi ya kuboresha miundombinu, matengenezo hayo yanaakisi dhamira ya kuendeleza usimamizi endelevu wa barabara. Mtandao imara wa barabara ni msingi wa ukuaji wa uchumi kwa kuwa unaunganisha wakulima na masoko, kusaidia shughuli za utalii na kuwezesha upatikanaji wa huduma za elimu na afya, alisisitiza Mhandisi Msangi.
Aidha, alibainisha kuwa barabara ya Iringa–Mtera ni muhimu kimkakati, kwani hutumika kusafirisha bidhaa kutoka mikoa ya Kusini kuelekea Kaskazini, na ni sehemu ya mtandao mkubwa wa barabara unaounganisha nchi za kusini na kaskazini mwa Afrika hadi Cairo, Misri.
Utekelezaji wa mradi huo unaonesha dhamira ya Serikali kupitia Mfuko wa Barabara kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu. Kutokana na hali bora ya barabara iliyoboreshwa, wananchi wanaoishi kandokando yake wanatarajia kunufaika na safari salama zaidi pamoja na kupanuka kwa fursa za kiuchumi.




