
Katika hatua ya kihistoria kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, chapa inayoongoza ya sukari nchini Tanzania, Bwana Sukari, chini ya kampuni ya Kilombero Sugar Company, imezindua rasmi sukari yake yenye vifungashio jijini Mwanza.
Uzinduzi huu unalenga kuleta unafuu wa bei, usafi, afya ya mlaji, na urahisi wa upatikanaji wa bidhaa hiyo, ikilinganishwa na sukari ya kupima inayotumika sana kwa sasa.
Kwa muda mrefu, wakazi wa Kanda ya Ziwa wamekumbwa na changamoto zinazotokana na matumizi ya sukari ya kupima. Mara nyingi, sukari ya kupima hupimwa kwa mizani inayotumika pia kwa bidhaa nyingine kama maharagwe na unga, hali inayosababisha wasiwasi kuhusu usafi wa sukari na usahihi wa vipimo. Matokeo ya changamoto hizi yamepelekea wateja wengi kupunguza uaminifu wao kwenye sukari ya kupima kwa kukosa uhakika wa kupata kiasi kamili kulingana na gharama wanazolipia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Wakili Mariam Abubakar Msengi, alisema, “Huu ni mchango mkubwa kwa ustawi wa wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa.
Uzinduzi huu unashughulikia changamoto za usafi na usahihi wa vipimo, na kutoa faida kubwa kwa wakazi wa Mwanza na kanda ya ziwa kwa ujumla.â€
Kwa upande wake, Fimbo Butallah, Mkurugenzi wa Biashara wa Kilombero Sugar Company, alieleza, “Uzinduzi huu ni hatua muhimu kwa Kanda ya Ziwa. Bwana Sukari si tu kwamba inatoa suluhisho la usafi na gharama nafuu, bali pia inazingatia sana afya na usalama wa mlaji wa bidhaa zetu.â€
Olympia Fraten, Meneja Biashara na Masoko wa Bwana Sukari, aliongeza kuwa, “Sukari yetu ya vifungashio ni suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazotokana na sukari ya kupima. Tunajivunia kuzingatia viwango vya juu vya usafi, usahihi, na unafuu ili kujenga uaminifu na kuhakikisha wateja wetu wameridhika.â€
Sukari yenye vifungashio kutoka Bwana Sukari sasa inapatikana katika soko la Mwanza na maeneo yote ya Kanda ya Ziwa, ikiwapa wakazi mbadala salama na wa kuaminika zaidi. Kuingia kwa bidhaa hii kunalenga kubadilisha uchaguzi wa wateja kutoka sukari ya kupima kwenda kwenye bidhaa bora zaidi huku ikiongeza viwango vya usafi na afya ya walaji katika kanda hiyo.