CAF yaitia adabu CS Sfaxien, Simba kunufaika

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeifungia CS Sfaxien ya Tunisia kucheza mechi mbili za kimataifa bila mashabiki baada ya vurugu dhidi ya CS Constantine ya Algeria.

Katika mechi hiyo, mashabiki wa Sfaxien walitupa mafataki, kitendo kilichopelekea adhabu ya kucheza bila mashabiki na faini ya Dola 50,000 (sawa na Sh. milioni 119).

Adhabu hiyo inanufaisha Simba SC, ambayo itakutana na CS Sfaxien Januari 5, 2024, nchini Tunisia, huku wenyeji wakiwa bila msaada wa mashabiki. Mechi nyingine ya Sfaxien bila mashabiki ni dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola Januari 19.

Vurugu zaidi zilizofanywa na Sfaxien katika mechi dhidi ya Simba, Desemba 15, zinatarajiwa kuleta adhabu zaidi. Katika mechi hiyo, mashabiki na wachezaji wa Sfaxien walizua tafrani baada ya Simba kushinda 2-1, bao la ushindi likifungwa na Kibu Denis dakika za mwisho.

Simba inajiandaa kuimarisha kikosi chake katika dirisha dogo la usajili, tayari ikiwa imemsajili winga Elie Mpanzu wa DR Congo. Kikosi cha Simba kinaelekea Singida leo kwa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars kesho.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 37, ikifuatiwa na Yanga (36), Azam FC (33), na Singida Black Stars (33).

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *