
BEKI wa kati wa Simba, Che Malone Fondoh, amesema kupoteza mchezo dhidi ya Yanga kumewaumiza lakini wanaamini zamu yao ya kufurahi haipo mbali kwa sababu kikosi chao kinaendelea kuimarika.
Malone, aliliambia gazeti hili viwango vya wachezaji wa Simba vinazidi ‘kupanda’ na anaamini mechi ya marudiano dhidi ya Yanga watapata ushindi.
“Mchezo dhidi ya Yanga umepita, najua mashabiki wameumia kama ambavyo na sisi wachezaji tulivyoumia, lakini timu yetu inaimarika na tunapambana, hatupo mbali na mafanikio,” alisema Fondoh.
Beki huyo alisema kwa sasa malengo yao ni kuhakikisha wanapata alama tatu katika kila mechi iliyoko mbele na hiyo inaendelea kupandisha viwango vyao.
“Hata ukiangalia mazingira ya goli tulilofungwa, ni bahati mbaya, lakini tumerejea mazoezini na kusahau yaliyopita na kupata ushindi mchezo wetu uliofuata dhidi ya Prisons…kwa sasa akili zetu tumeelekeza kuikabili Namungo,” alisema Malone.
Nyota huyo ndiye alifunga bao pekee katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine na Malone alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Simba leo itakuwa mwenyeji wa Namungo FC kwenye Uwanja wa KMC, Complex Dar es Salaam.
Chanzo: Nipashe