Thursday, December 18, 2025
spot_img
HomeMichezoChristian Bella apewa uraia wa Tanzania

Christian Bella apewa uraia wa Tanzania

Msanii maarufu wa muziki wa Bongofleva mwenye ladha ya R&B na Afro-pop, Christian Bella, amepewa rasmi uraia wa Tanzania.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Simbachawene amesema Tanzania ina idadi kubwa ya wahamiaji na kwamba baadhi yao wamekuwa wakipewa uraia baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa kisheria. Amesema uamuzi wa kumpa Bella uraia umetokana na mchango wake, mwenendo wake mzuri na utii wake kwa sheria za nchi.

“Sasa anakwenda wapi, amekwisha fika. Ameoa hapa, ana watoto hapa na atapata wajukuu hapa. Anafanya kazi vizuri, hana makosa, amefuata utaratibu na muda wote alioishi hapa amelipa malipo stahiki, siyo wengine wanaolanda landa tu,” amesema Simbachawene.

Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa utoaji wa uraia ni mchakato unaozingatia usalama wa taifa, akieleza kuwa uraia unaweza kufutwa endapo mhusika hatatii sheria na taratibu zilizopo.

“Hatuwezi kumpa uraia mtu ambaye ni hatari au anayeweza kugeuka kuwa hatari. Ndiyo maana kuna mchakato wa uhakiki (vetting) unaofanyika kabla ya mtu kupewa uraia,” ameongeza.

Kwa upande wake, Christian Bella awali alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini ameishi Tanzania kwa muda mrefu akijishughulisha na shughuli za kisanii na kuwa mmoja wa wasanii waliopata mashabiki wengi nchini kutokana na kazi zake za muziki.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments