
Timu ya Watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) hivi karibuni imefanya ziara katika maeneo ya Temeke na Tabata kwa lengo la kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji.
Ziara hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Mkama Bwire, ililenga kutathmini maendeleo ya huduma ya maji katika maeneo yaliyokuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu.
Miongoni mwa maeneo yaliyochunguzwa ni Soweto, Azimio, Kichangani, Mtongani, Kwa Gude, Lumo, Ikizu Kigilagila, na viwanda vya Pepsi na Sigara Temeke. Katika eneo la Tabata, walitembelea Bush Road Makuburi na Tawi la Yanga.

Wakati wa ziara, timu hiyo ilishuhudia mabadiliko chanya katika huduma ya maji, ambapo huduma hiyo imeimarika na kuweza kuwafikia wananchi zaidi. Mhandisi Bwire alisema, “Tunaendelea kufanya kazi kwa karibu na jamii ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya maji.”
DAWASA pia imejizatiti katika kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Katika juhudi za kuboresha mawasiliano na wananchi, mamlaka hiyo imetoa wito kwa wananchi wanaokutana na changamoto za huduma kuwasiliana nao moja kwa moja kupitia nambari ya simu 0800110064 bila malipo, au kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia WhatsApp kwenye 0735 202121.

