Katika kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imezidi kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kufungua dawati maalum la huduma kwa wateja katika mtaa wa Bwawani, Stand ya Makumbusho. Hatua hii inalenga kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kupokea maoni yatakayosaidia kuboresha huduma ya maji jijini.
Akizungumza katika dawati hilo, Afisa Huduma kwa Wateja wa DAWASA, Ndugu Veronica Sebastian, amesema kuwa zoezi hilo linafanyika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, likiwa na lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja, hususan wanawake ambao ndio watumiaji wakuu wa huduma ya maji katika familia nyingi.
“Katika dawati letu hapa Stendi ya Mabasi Makumbusho, mwananchi anaweza kupata huduma zote zinazotolewa na Mamlaka. Hizi ni pamoja na maunganisho mapya ya maji, utatuzi wa changamoto za bili, kushughulikia uvujaji, pamoja na kupatiwa elimu kuhusu njia mbalimbali za malipo ya huduma za DAWASA. Pia tunapokea maoni ya wananchi kuhusu namna ya kuboresha zaidi huduma zetu,” amesema Veronica.
Ameongeza kuwa dawati hilo litatoa huduma kwa siku tano, kuanzia tarehe 3 Machi 2026 hadi 7 Machi 2026, na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo, hasa wanawake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bwawani, Ndugu Mahmood Tonsa, ameipongeza DAWASA kwa kuwafuata wananchi mtaani na kuwasikiliza moja kwa moja. Amesema hatua hiyo ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za umma.
“Tunashukuru kwa huduma ya maji tunayoendelea kuipata katika mtaa wetu wa Bwawani. Ingawa zipo changamoto ndogondogo zinazolalamikiwa na wananchi, hii ni fursa adhimu kwao kufika katika banda hili na kupatiwa ufumbuzi. Binafsi nimejionea elimu na huduma inayotolewa hapa ni bora sana,” amesema Tonsa.
Naye mkazi wa Sinza A, Kidani Magwille, ameonesha kuridhishwa na huduma aliyoipata katika dawati hilo. Amesema alifika na changamoto ya bili ya maji pamoja na mita yake kuwa na ukungu, na alifanikiwa kutatuliwa papo hapo.
“Nimefarijika kuona changamoto yangu imeshughulikiwa mara moja. Huu ni msaada mkubwa kwa wananchi, hasa sisi wanawake ambao ni watumiaji wakubwa wa maji majumbani,” amesema Kidani.
Hatua hii ya DAWASA inaonesha dhamira ya Mamlaka katika kuboresha huduma kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi, huku ikiweka mkazo katika kuwainua na kuwajumuisha wanawake katika upatikanaji wa huduma bora za maji.







