Dk. Mhede aongoza zoezi la uchanjaji wa mifugo Iringa


 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Edwin Mhede, ameongoza zoezi la utambuzi na uchanjaji wa mifugo mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Utoaji Chanjo kwa Mifugo iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa mkoani Simiyu hivi karibuni. 

Akizungumza Julai 3, 2025, mkoani Iringa, Dk. Mhede amesema kuwa kampeni hiyo ya miaka mitano inalenga kuchanja mifugo yote nchini kama sehemu ya uwekezaji katika sekta ya mifugo, unaowaletea faida wafugaji na kukuza uchumi wa taifa.

 “Tunalenga kuchanja ng’ombe wapatao 400,000 hapa Iringa, ambapo leo tumetambua na kuchanja ng’ombe wapatao 1223 ambapo kwenye shamba la Kibete tumechanja ng’ombe 720 na Kijiji cha Kalenga ng’ombe 603  na tayari tumejiridhisha kuwa chanjo zipo za kutosha na tumeanza kutembelea maeneo mbalimbali kama vile Kijiji cha Kalenga na Shamba la Mifugo la Kibebe linalomilikiwa na  Richard Philips ili kuhakikisha zoezi linaenda vizuri,” amesema Dkt. Mhede.

 Mbali na ng’ombe, Dk. Mhede amesema chanjo pia zitatolewa kwa kuku, na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwani huduma hiyo inatolewa kwa gharama nafuu kutokana na ruzuku ya serikali.

Aidha, Dk. Mhede amesema utekelezaji wa kampeni hii unakwenda sambamba na juhudi za serikali za kufungua masoko ya ndani na nje kwa mifugo na mazao yake.

 Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Iringa,  Kheri James, amesema kuwa Serikali ya mkoa inatoa ushirikiano wa karibu na wizara katika kuhakikisha kampeni ya chanjo inafanikiwa, amesisitiza kuwa afya ya mifugo ni msingi wa ustawi wa jamii nyingi mkoani humo.

 “Wafugaji wengi wa Iringa wanategemea mifugo   kujiingizia kipato na mahitaji ya chakula aina ya protini ili wananchi kupata mlo kamili tunapongeza juhudi za Serikali kupitia Wizara kwa kuhakikisha mifugo inapata chanjo stahiki kwa gharama nafuu,” amesema.

Ameongeza kuwa Mkoa wamejipanga kuhakikisha kila halmashauri inashiriki kikamilifu kwenye zoezi la uchanjaji wa mifugo.

Kwa upande wake, Ofisa Mifugo wa Mkoa wa Iringa, Hamadi Mwansasu, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa mkoa umepokea chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, pamoja na chanjo za kuku dhidi ya kideri, mafua, na ndui.

 Amebainisha kuwa tayari timu ya wataalamu ipo kazini kuhakikisha zoezi linafanyika kwa ufanisi katika halmashauri zote za Mkoa wa Iringa.

Kwa mujibu wa Mwansasu, matarajio ni kwamba tija ya uzalishaji wa mifugo itaongezeka na hivyo kuwasaidia wafugaji kupata kipato zaidi na kuboresha maisha yao.

Katibu wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Iringa, Felix Sanga, aliipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa mifugo, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vya mifugo na kuongeza uzalishaji.

Mkurugenzi wa Shamba la Mifugo la Kibebe, Richard Philips, amesema shamba lake limeshiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwataka wafugaji wengine wachangamkie fursa hiyo. Aliongeza kuwa serikali imeahidi kuongeza aina zaidi za chanjo kwa lengo la kulinda afya ya mifugo.

Miongoni mwa wafugaji walionufaika na zoezi hilo ni Donard Luhavi kutoka Kijiji cha Kalenga, amesema mpango huo utaimarisha afya ya mifugo na kuongeza thamani ya mauzo yao.

“Gharama ya chanjo imepunguzwa kutoka shilingi 1,000 hadi 500 kwa kila ng’ombe. Hii imetupa motisha zaidi ya kushiriki kikamilifu katika zoezi hili,” amesema Luhavi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *