📌Ni ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme chenye uwezo wa MVA 60.
📌Mradi kugharimu takribani bilioni 44.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba leo Februari 13, 2026 amekagua na kuweka jiwe la msingi la Mradi wa ujenzi kituo cha kupokea na kupoza umeme cha MVA 60 Mkatata Tanga na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 33.
Akiweka jiwe la msingi mradi huo, Dk. Mwigulu amesema kutekelezwa kwa mradi huo ni jitihada za Rais Samia kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.
“Nitoe rai kwa Wizara ya Nishati kuhakikisha kasi ya ukamilishwaji wa mradi huo na unakamilika kwa wakati “. amesisitiza Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine ameiagiza Wizara ya Nishati kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi takribani Sh. bilioni moja.




Ujennzi wa mradi huo ni Sh. bilioni 44 na unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme vyenye uwezo wa MVA 60 huku kila kimoja kikiwa na MVA 30, pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo cha Mkata hadi kwa Msisi.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemshukuru Rais Samia kwa kuwezisha upatikanaji wa fedha zitakazo tumika katika utekelezaji wa mradi huo.
“Utekelezaji wa mradi huu unakwenda kuondoa changamoto za umeme katika Wilaya za Handeni na Kilindi ambazo zinapata umeme kutokea Tanga mjiani ambapo ni umbali mrefu”. amesema Ndejembi.
Amefafanua kuwa kupitia miundombinu hiyo mipya, umeme utasafirishwa kutoka Mkata kwenda Msisi kwa umbali wa kilomita 45, hatua itakayoongeza uwezo wa usambazaji na kuimarisha huduma katika maeneo hayo.
Kuimalika kwa huduma ya umeme Wilaya za Handeni na Kilindi kutachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.








