Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo chama chake kitapata ridhaa ya kuwaongoza tena Wazanzibari, serikali yake itaendeleza dhana ya uongozi unaoacha alama.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo leo, Septemba 12, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari visiwani humo kuelekea uzinduzi wa kampeni za CCM.
Amesema anatarajia kuona wagombea wote wakiendesha kampeni zenye kulenga sera na hoja zenye manufaa kwa wananchi, badala ya matusi, chuki au mifarakano. โNi lazima kuhubiri amani ya nchi, kwani bila ya amani hakuna maendeleo,โ alisema.
Ameongeza kuwa CCM itaendesha kampeni za kistaarabu, zikijikita katika kuhimiza mshikamano, umoja na amani ya taifa.
Bima ya afya kwa wote kipaumbele cha Dk. Mwinyi
Katika hatua nyingine, Dk. Mwinyi amesema iwapo CCM itapewa ridhaa nyingine ya kuongoza, serikali yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ili kuimarisha huduma za afya nchini.
Amesema bima hiyo itakuwa suluhisho la kudumu katika kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuwapa madaktari nafasi ya kutoa huduma bora kwa ufanisi zaidi.
โBima ya afya kwa wote ndiyo ufumbuzi wa changamoto ya madaktari kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja. Kupitia mfuko wa afya tutahakikisha wananchi wote wanapata huduma bila vikwazo,โ alisema Dk. Mwinyi.




