Dk. Rutachunzibwa: Mtanzania wa kwanza kutibu saratani bila upasuaji

Dk. Fredy Rutachunzibwa wa Hospitali ya Kairuki ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kufuzu mafunzo ya kutibu saratani kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound).

Teknolojia hiyo inatoa tiba isiyo ya upasuaji kwa kutumia mawimbi ya sauti yenye nguvu kuteketeza seli za saratani kwa usahihi.

Akizungumza leo Dk. Rutachunzibwa ameeleza kuwa HIFU inapunguza maumivu, hatari ya maambukizi, na muda wa kupona kwa wagonjwa.

“Matibabu haya hayaingizi chochote ndani ya mwili; ngozi haiguswi, hakuna nusu kaputi, na mgonjwa anaondolewa uvimbe huku akiwasiliana na daktari,” amesema.

Hospitali ya Kairuki imeandika historia kama kituo cha kwanza nchini Tanzania, Afrika Mashariki, na Kati kutumia teknolojia hii, ikiwa ni ya tatu barani Afrika. Dk. Rutachunzibwa, aliyepata mafunzo hayo nchini China mwaka jana, amesema kuwa HIFU inafaa kwa saratani za aina mbalimbali na inatoa suluhisho kwa wagonjwa wengi waliokuwa wakikosa matibabu ya kisasa kutokana na changamoto za kifedha au umbali wa hospitali.

“Kinachofanyika ni kwamba mawimbi ya sauti yanapelekwa katika eneo lenye uvimbe na kuuteketeza bila kuathiri maeneo mengine,” ameeleza.

Dk. Rutachunzibwa amesisitiza kuwa teknolojia hiyo ni hatua kubwa katika mapinduzi ya sekta ya afya nchini Tanzania. “Matibabu haya yalikuwa yakipatikana tu katika mataifa yaliyoendelea, lakini sasa yanapatikana hapa Hospitali ya Kairuki. Hii ni hatua muhimu katika kupunguza vifo vya saratani na kuongeza ufikiaji wa huduma za kisasa za afya,” amesema.

Kwa teknolojia ya HIFU, Tanzania imeingia katika ramani ya matibabu ya kisasa, hatua inayotoa matumaini mapya kwa wagonjwa wa saratani nchini na katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *