Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wa Serikali yake kutoa ruzuku ya chanjo, unalenga kuvuna soko la mifugo hai na nyama kimataifa.
Dk Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi Oktoba 4, 2025 alipozungumza na wananchi wa Babati mkoani Manyara, katika mkutano wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Amesema Serikali ilifanya uamuzi wa kutoa ruzuku ya chanjo itakayolinda afya ya wanyama na soko la kimataifa ambalo awali Tanzania ililipata lakini ilishindwa kupeleka bidhaa kwa sababu haikuwa kwenye rekodi za kimataifa kuhusu usalama wa wanyama wake.
“Soko lile tutapeleka au wanyama hai, au nyama au mazao mengine ya mifugo. Lakini ilikuwa tuthibitishwe kwanza kwamba Tanzania tumeingia kwenye orodha ambayo tunafuga na mifugo yetu ni salama,” amesema.
Ameahidi kuendelea kusimamia ufugaji Tanzania na kufungua zaidi fursa ili wafugaji wanufaike na masoko ya nje ya nchi.










