Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan amesema ndani ya mwezi mmoja Serikali itafungua vituo vya kununulia mahindi katika eneo la Makambako mkoani Njombe.
Hatua hiyo, inajibu changamoto iliyokuwepo kwa wakulima wa mahindi katika eneo hilo, ambalo mara kadhaa wamekuwa wakilalamikia kuwepo kituo cha kununua zao hilo Makambako.
Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi Septemba 6, 2025 alipozungumza na wananchi wa Makambako mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya mikutano yake ya kampeni za urais.
“Nataka niwape habari njema, ndani ya mwezi huu, pengine kuanzia wiki ijayo, tutafungua vituo vya kununua mahindi ndani ya mkoa huu wa Njombe,” amesema.
Sambamba na hilo, Dk. Samia amesema yupo tayari kupokea andiko la pendekezo la utekelezaji wa mradi wa umeme wa upepo katika eneo la Makambako, kwani ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya matumizi ya nishati safi.
Katika mkutano wake huo, ameahidi kuangalia uwezekano wa kujenga bandari kavu katika eneo hilo au kwingine popote alikopokea maombi hayo.










