Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itatumia rasilimali zake za ndani ili kupata fedha za kutekeleza miradi iliyopangwa.
Msingi wa kauli hiyo ni kile alichoeleza, muhula uliopita Serikali ilikuwa inapata mikopo kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo za fedha za kimataifa.
Hata hivyo, amefafanua kwa kile kilichotokea hivi karibuni (vurugu za Oktoba 29), huenda kikaipunguzia sifa Tanzania kupata fedha hizo kwa urahisi.
Dk Samia ameeleza hayo Novemba 18, 2025 katika uapisho wa mawaziri na manaibu mawaziri Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
“Rasilimali ni chache, mara nyingine tunategemea kutoka nje, lakini yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo, huenda yakatupunguzia sifa ya kupata mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza wa awamu hii.
“Muhula kwanza tulipata sana kwa sifa zetu, msimamo wetu na kazi tunazozifanya. Lakini doa tulilolitia huenda likaturudisha nyuma, kwa maana hiyo tuna kazi ya kutafuta fredha humu ndani,” ameeleza.
Mkuu huyo wa nchi, amesisitiza Serikali itatumia rasilimali iliyobarikiwa, sambamba na kuangalia njia zitakatumika ili kupata fedha ya kutekeleza miradi iliyopangwa.




