Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo, Serikali yake itajikita katika kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Amesema atalitekeleza hilo, kwa kuhakikisha anawaandalia wananchi mazingira ya kuwa na shughuli za kufanya ili waingize vipato na kuinua ustawi wa maisha yao.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Septemba 18, 2025, alipozungumza na wananchi wa Nungwi visiwani Zanzibar, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
Amesema ahadi ya CCM katika miaka mitano ijayo, ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua hali za maisha ya wote, kuimarisha ustawi wa jamii, kulinda amani, usalama na utulivu na kujenga taifa linalojitegemea.
“Katika kujenga Taifa linalojitegemea, hatutafika huko mpaka kila mtu ndani ya Tanzania, kila kijana awe na shughuli inayompa kipato, yeye mwenyewe asimame kama mtu mmoja ajitegemee, alafu kwa ujumla wetu tutaweza kujitegemea,” amesema.




