Sunday, October 12, 2025
spot_img
HomeAfyaDkt Samia: Nitaweka nguvu huduma za mama na mtoto

Dkt Samia: Nitaweka nguvu huduma za mama na mtoto

Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.Samia Suluhu Hassan amewaahidi wananchi wa Simiyu kuendeleza kasi ya uboreshaji wa sekta ya afya, ikiwemo kuongeza nguvu katika huduma za mama na mtoto.

Dk Samia ameeleza hayo, leo Oktoba 9,2025 Alhamisi wakati aliposimama kuzungumza na wananchi wa Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu katika mwendelezo wa kampeni za kusaka kura.

“Tutaendelea na kasi ileile ya huduma za afya, tutajenga vituo vya afya na zahanati zaidi na tunakwenda kuboresha hospitali ya wilaya kwa kujenga jengo kubwa la mama na mtoto, ili huduma ziendelee kwa kiasi kikubwa,”

“Mimi ni mama, najua masuala ya kujifungua kazi yake, huduma zinazotakiwa, hivyo naweka nguvu huko kwa mama na mtoto,” amesema Dk. Samia.

Mbali na hilo, Dk. Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM amewaambia wananchi Lamadi, kuwa atakwenda kuongeza shule za sekondari na msingi, sambamba na vyuo vya ufundi wa Veta ili vijana kupata mafunzo ya ufundi yatakayowaweza kujiajiri na kuajiriwa.

“Kwenye maji kazi kubwa imefanyika, tunatambua baadhi ya maeneo kuna miundombinu imechakaa, inahitaji kufanyiwa kazi, nimeongozana na Waziri wa Maji (Jumaa Aweso) amesikia tunakwenda kuifanyia kazi,”

“Tunakwenda kumaliza vitongoji vilivyobaki katika sekta ya umeme, Ilani iliyopita iliagiza kupeleka umeme kwenye vijiji tu sasa, tumejiongeza hadi vitongoji. Mkituchagua tena tunakwenda kumaliza vitongoji,” amesema Dk. Samia.

Ujenzi wa barabara hautasimama

Katika mkutano huo, Dk. Samia amewaahidi Watanzania kuwa ujenzi wa Barabara unaondelea katika maeneo mbalimbali hautasimama, akisema miundombinu hiyo itajengwa kama ambavyo imeanishwa katika Ilani.

Ahadi ya soko

Katika mazungumzo yake, Dk. Samia alikumbushia ahadi yake ya ujenzi wa soko, alipofanya ziara wilayani humo, miezi iliyopita akisema akiahidi lazima atekeleze.

“Nilitenga fedha za kujenga soko la hapa Lamadi, lakini uongozi wa halmashauri unabishana lijengwe Lamadi au Nyashimo, ndio maana soko halikujengwa. Lakini ahadi yangu bado iko palepale, madiwani wakielewana,” ameeleza Dk Samia.

Hata hivyo, Dk. Samia amesisitiza kuwa ahadi yake, soko lijengwe Lamadi na stendi ya mabasi ijengwe eneo la Nyashimo,kupitia mradi wa uboreshaji wa miji utakaofanya shughuli hizo.

Tujitokeza Oktoba 29

Dk. Samia amewaomba wananchi wa Simiyu waliojindikisha katika Daftari wa Wapigakura kujitokeza kushiriki mchakato huo.

“Kama ni baba au mama wa familia, hakikisha kila aliyejiandikisha katika nyumba yako anajitokeza kupiga kura,”

“Kama ni balozi hakikisha watu wa eneo lako, wote walioandikishwa wametoka kupiga kura. Tukakigie kura CCM, bado tuna mengi tunayahitaji,” amesema Dk. Samia.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments