Saturday, November 8, 2025
spot_img
HomeHabariRC Chalamila aagiza DAWASA kuboresha huduma ya maji Dar

RC Chalamila aagiza DAWASA kuboresha huduma ya maji Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kuweka mikakati ya haraka ya kuboresha huduma hiyo.

Chalamila ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kifupi na watendaji wa DAWASA kilicholenga kufanya tathmini ya upatikanaji wa maji, kwa kubaini maeneo yenye changamoto za muda mrefu ili kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.

Amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa, ikiwemo Mradi wa Maji wa Dar es Salaam Kusini (Bangulo), ambao umekamilika na tayari umeanza kutoa huduma katika maeneo ya Segerea, Kinyerezi, Kibamba na Ubungo — yaliyokuwa yakikabiliwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu.

“Nikiri kweli kuna maeneo mengi ya Dar es Salaam ambayo yanakabiliwa na upatikanaji mdogo wa maji. Nitoe rai kwa wananchi wa maeneo hayo kuwa na subira wakati Serikali kupitia DAWASA ikichukua hatua za haraka kuhakikisha huduma inaboreshwa,” amesema Chalamila.

Ameeleza kuwa hatua nyingine inayochukuliwa na Serikali ni kuimarisha matumizi ya visima zaidi ya 190 vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, ambapo DAWASA imeanza kuvihusisha rasmi katika mfumo wa usambazaji maji ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema mamlaka imepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na tayari inaendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha huduma ya maji jijini.

Amesema mahitaji ya maji katika eneo la huduma la DAWASA yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na ongezeko la watu mjini, ambapo sasa yanakadiriwa kufikia mita za ujazo 685,677 kwa siku, ikilinganishwa na uzalishaji wa sasa wa mita za ujazo 534,600 kwa siku.

“Jitihada kubwa zimefanyika na Serikali kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa maji, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa maji Bangulo unaotoa huduma kwa wakazi wa Segerea, Ukonga, Kisarawe na maeneo ya Kinyerezi ambayo hapo awali yalikuwa na changamoto kubwa ya huduma hiyo,” amesema Mhandisi Bwire.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments