Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake katika miaka mitano ijayo, itafunga mitambo mipya katika kiwanda cha kuchakato zao la chai wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Sambamba na hilo, ameahidi kuanzisha ujenzi wa mradi wa Bandari Kavu katika eneo la Old Korogwe wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika Bandari ya Tanga.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Septemba 30, 2025 alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
Amesema Serikali yake imepanga kufunga mitambo mipya ya kuchakata zao la chai na kiwanda hicho, kitaendeshwa na ushirika wa eneo hilo, chini ya utasimamiwa na Bodi ya Chai Tanzania.
Pia, ameahidi kuanzishwa ujenzi wa bandari kavu wilayani humo, ikiwa ni kutimiza ombi la wananchi wa eneo hilo na kupunguza msongamano wa magari katika Bandari ya Tanga.
“Hatujasahau pendekezo la kuanzishwa Bandari Kavu katika eneo la Old Korogwe. Na hii ni kwa ajili ya kuondoa msongamano wa magari katika Bandari ya Tanga, ambako shughuli zimeongezeka sana kufuatia maboresho tuliyoyafanya, hili nalo tutakwenda kulifanyia kazi,” amesema.




