Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo mpya za mwezi Machi 2026.
Katika marekebisho hayo, watumiaji wa dizeli wameathirika zaidi ikilinganishwa na wale wa petroli na mafuta ya taa. Ongezeko hilo linagusa mafuta yanayoingizwa kupitia Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Kuanzia Machi 4, 2026, bei ya rejareja ya petroli jijini Dar es Salaam imeongezeka hadi Sh. 2,864 kwa lita kutoka Sh. 2,788 ya Februari, ikiwa ni ongezeko la Sh. 76. Dizeli imepanda kwa Sh. 157 hadi Sh. 2,858 kutoka Sh. 2,701, huku mafuta ya taa yakiongezeka kwa Sh. 186 hadi Sh. 2,932 kutoka Sh. 2,746.
Hali kama hiyo imejitokeza Tanga, ambapo petroli sasa inauzwa Sh. 2,925 kwa lita kutoka Sh. 2,849, dizeli Sh. 2,919 kutoka Sh. 2,762 (ongezeko la Sh. 157), na mafuta ya taa Sh. 2,993 kutoka Sh. 2,807 (ongezeko la Sh. 186).
Mtwara nako mwenendo ni huo huo; petroli imeongezeka kwa Sh. 75 hadi Sh. 2,956 kutoka Sh. 2,881, dizeli imepanda kwa Sh. 157 hadi Sh. 2,951 kutoka Sh. 2,794, na mafuta ya taa yameongezeka kwa Sh. 187 hadi Sh. 3,025 kutoka Sh. 2,838.
Taarifa ya Ewura inaonyesha kuwa kwa ujumla dizeli na mafuta ya taa vimepanda kwa kiwango kikubwa zaidi ya petroli katika bandari zote tatu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk. James Andilile, bei za bidhaa hizo katika soko la Ghuba ya Uarabuni zimeongezeka kwa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 9.8 kwa dizeli na asilimia 7.4 kwa mafuta ya taa katika mwezi Machi.
Aidha, gharama za uagizaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 0.07 kwa petroli, asilimia 10.76 kwa dizeli, huku mafuta ya taa yakionyesha upungufu wa asilimia 5.41. Hakukuwa na mabadiliko ya gharama za uagizaji katika bandari za Tanga na Mtwara.
Mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha pia yameongeza shinikizo, baada ya kiwango kinachotumika mwezi Machi kuongezeka kwa asilimia 8.54.
Licha ya changamoto zinazoendelea Mashariki ya Kati zinazoathiri masoko ya mafuta duniani, Ewura imeeleza kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta kuendeleza shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mamlaka hiyo imewaonya wauzaji wa rejareja na jumla kuzingatia kikamilifu bei kikomo zilizotangazwa, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka utaratibu wa bei.
“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei katika mabango yanayoonekana wazi, yakionesha bei za mafuta, punguzo au vivutio vya kibiashara vinavyotolewa. Wateja wanashauriwa kununua katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kuchochea ushindani,” imeeleza taarifa hiyo.
Ni kosa kuuza mafuta bila kuonesha bei bayana, na adhabu kali zitatolewa kwa watakaokiuka masharti hayo ya kisheria.
Pia, wauzaji wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), huku wanunuzi wakishauriwa kudai stakabadhi zinazoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta na bei kwa lita. Stakabadhi hizo zitasaidia endapo kutatokea malalamiko ya bei au ubora, pamoja na kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali.




