
Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira nchini zimeelekezwa kutoa taarifa sahihi kuhusu uendeshaji na utoaji wa huduma kwa kuwa taarifa hizo hutumika katika utekelezaji wa mipango ya Serikali inayolenga kuimarisha sekta ya maji nchini.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dk. James Andilile, wakati akifungua kikao kazi cha kuhakiki taarifa kwa watendaji wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira za Wilaya na Mijimidogo, jijini Dodoma.
Dk. Andilile amesema kuwa, EWURA imetathmini taarifa zote zilizowasilishwa na Mamlaka hizo katika mfumo wa Maji kwa Mwaka 2023/24 na kubaini takwimu zisizo sahihi za kiwango cha maji yanayozalishwa, muda wa upatikanaji wa huduma, usimamizi wa usafi wa mazingira,hali ya upatikanaji na kiwango cha uhitaji wa maji,ubora wa maji pamoja na upotevu wa maji.
