
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameulalamikia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, akisema hauko kwenye ubora, huku akisema viwanja vitatu tu vinavyobeba taswira ya soka la Tanzania ni ule wa Benjamin Mkapa, Azam Complex, ambavyo vyote vipo, Dar es Salaam na New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yake na Coastal Union, akiibuka na ushindi wa bao 1-0 lililowekwa wavuni na Jean Baleke, Gamondi amesema, baadhi ya viwanja ni vibovu kiasi kwamba vinasababisha timu zicheze mpira wa kubutuabutua kitu ambacho si picha nzuri kwa Ligi ya Tanzania.
“Pointi hizi tatu ni muhimu sana kwetu katika mwendelezo wa kupigania nafasi ya kutwaa ubingwa, lakini sijafurahishwa na hali ya uwanja, pamoja na baadhi ya maamuzi ya mwamuzi.
Kwa wachezaji wakubwa na ligi bora huwezi kucheza mpira kwenye uwanja kama huu, haikuwa mbaya kwa upande wetu, hata Coastal Union walikuwa wakipiga mipira mirefu, walijaribu kama mara mbili tatu kuanzia mpira nyuma wakashindwa na kuanza kubutua na hii si picha nzuri kwa Ligi ya Tanzania, kwangu mimi, Uwanja wa Azam Copmlex, New Amaan Zanzibar na Benjamin Mkapa, ndivyo vinavyobeba taswira njema ya ligi ya hapa nchini,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, hakufafanua juu ya maamuzi mabaya ya waamuzi waliochezesha mchezo huo.
Akiuzungumzia mchezo huo, raia huyo ya Argentina, alisema kipindi cha kwanza hawakuwa bora, lakini walibadilika cha pili.
“Kipindi cha kwanza hatukutengeneza nafasi, lakini cha pili tulibadilika, nadhani mabadiliko tuliyoyafanya yalitufanya kuwe salama zaidi, tulitengeneza nafasi na kufunga bao lingine,” alisema Gamondi.
Kocha mpya wa Coastal Union, Juma Mwambusi, ambaye alikuwa benchini kwa mara ya kwanza, aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana, akisema Yanga walinufaika na ubora wa mchezaji mmoja mmoja.
“Nashukuru wachezaji wangu wamepambana sana, tumepoteza nafasi mbili za wazi kipindi cha kwanza, hawakuwa makini, niliwaambia kuwa watulivu wanapofika langoni, lakini naona bado, hili ni lazima nilifanyie kazi.
“Yanga wametumia ule ubora wa mchezaji mmoja mmoja kuamua matokeo, vinginevyo hii mechi ingeisha kwa sare, tumekubali, nitakwenda kukaa na wachezaji, ili kukiboresha kikosi,” alisema Mwambusi.
Kuhusu hali ya uwanja, alisema ulikuwa sawa na wala haoni tatizo na hivyo ndivyo viwanja vya Tanzania vilivyo.
“Uwanja uko sawa, hivi ndivyo viwanja vyetu na wao wameshinda kwenye uwanja huu huu, wangefungwa sijui wangesemaje,” alisema kocha huyo.
Ushindi huo umewapeleka Yanga nafasi ya pili ikifikisha pointi 21, ikicheza michezo saba ikishinda yote, bila kuruhusu bao, huku Coastal, ikiwa nafasi ya 11, ikikusanya pointi nane kwa michezo tisa iliyocheza, ikishinda miwili, sare miwili na kupoteza mitano.
Chanzo:Nipashe