
BAADA ya kucheza michezo mitano bila kupoteza, hatimaye Mtibwa Sugar, juzi, ilipata mbabe wake kwenye Ligi ya Champioship, ilipochapwa bao 1-0 dhidi Geita Gold katika mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa, Uwanja wa Nyankumbu, Geita.
Mechi hiyo ilikumbushia enzi zao zilipokuwa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani zote ziliteremka msimu uliopita, hivyo kuwa ni mechi yenye upinzani mkali.
Bao pekee la ushindi la Geita Gold lilifungwa na straika wa zamani wa Stand United, Ndanda, Simba, KMC, Polisi Dodoma na Mtibwa Sugar yenyewe, Vitalisy Mayanga, dakika ya 38, ambaye alipiga mpira kwa kichwa cha kuchupa kutokana na mpira uliorushwa na beki wa zamani wa Yanga, Abdulaziz Makame.
Kipigo hicho si tu kwamba kinahitimisha Mtibwa Sugar kucheza michezo mitano bila kupoteza, lakini kimeishusha kutoka nafasi ya kwanza mpaka ya pili.
Ushindi huo unaipeleka Geita Gold kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikifikisha pointi 14 kwa michezo sita iliyocheza, ikishinda minne na sare miwili, huku Mtibwa ikisalia na pointi 13 kwa michezo sita, ikishinda minne, sare moja na kupoteza mmoja.
Kwingineko, Maafande wa Polisi Tanzania waliendeleza ubabe wao baada ya kuichapa African Sports bao 1-0 kwenye Uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro ambao umeipeleka hadi nafasi ya saba ya msimamo ikifikisha pointi nane, ikiiacha African Sports hoi kwenye nafasi ya 15 na pointi yake moja kwa michezo sita iliyocheza.
Kwenye Uwanja wa Sokoine, wenyeji, Mbeya City walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbuni, lililowekwa ndani ya wavu na Andrea Kihumbi dakika ya 39 ya mchezo.
Ushindi huo unaipandisha Mbeya City hadi nafasi ya tano, ikifikisha pointi 11, huku Mbuni ikisalia na pointi sita ikiwa nafasi ya 11 ya msimamo.
Chanzo:Nipashe