HESLB yawapangia mikopo wanafunzi elimu ya juu 9,000 awamu ya 4

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetangaza awamu ya nne yenye wanafunzi 9,068 wa shahada ya awali na stashahada (diploma) waliopangiwa mikopo yenye thamani bilioni 27.52 kwa mwaka wa masomo 2024/25.

Wanafunzi 4,400 wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo nchini kwa ajili ya masomo ya shahada za awali, wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 13.74 bilioni. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika tovuti rasmi ya HESLB, awamu hii pia imewajumuisha wanafunzi 2,646 wa shahada ya awali wanaoendelea na masomo ambao wamepangiwa mikopo kwa mara ya kwanza (first-time continuing) yenye thamani Sh. bilioni 8.37.

Katika awamu ya nne iliyotangazwa, wamo pia wanafunzi wapya 2,022 wa stashahada wa mwaka wa kwanza ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 5.41. Wanafunzi hao wamedahiliwa katika programu za kipaumbele katika vyuo mbalimbali vya kati nchini.

Kwa mujibu wa HESLB, kupitia ruzuku ya ‘Samia Scholarship’ mpaka sasa, jumla ya Sh. bilioni 3.14 zimetolewa kwa ajili ya ruzuku kwa wanafunzi 625; (588 awamu ya kwanza, 11 awamu ya pili na 26 awamu ya tatu) kwa wanafunzi wa shahada ya awali, mwaka wa kwanza wanaonufaika na ‘Samia Scholarship’ kwa mwaka wa masomo 2024/25 katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati na tiba.

Kuhusu kufunguliwa Dirisha la Rufani 2024/25, HESLB imeeleza kuwa wanafunzi walioomba mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/25 lakini hawakuridhika na viwango vya awali walivyopangiwa au hawajapangiwa mikopo, wanashauriwa kukata rufani ndani ya siku saba kuanzia Jumatatu Novemba 4 hadi Jumapili
 Novemba 10 mwaka huu.

Serikali kupitia HESLB, mwaka huu wa masomo inatarajiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 787 kwa wanafunzi 250,000.

Hilo ni ongezeko la wanafunzi 25,944 kulinganishwa na wanufaika 224,056 wa mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *