Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema kikosi chake kinaendelea kuimarika licha ya kutokuwa kamili kutokana na baadhi ya wachezaji wake kushiriki mashindano ya CHAN.

Azam ilipata ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Polisi Rwanda baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Nyamirambo.
Ibenge amesema michezo ya kirafiki inayochezwa Rwanda itamsaidia kuandaa mfumo na kikosi bora kuelekea msimu mpya, huku akisisitiza malengo makubwa ya Azam ni kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Klabu hiyo haijawahi kutinga hatua hiyo tangu iingie Ligi Kuu mwaka 2008/09.
Kocha huyo mwenye mafanikio makubwa kimataifa aliwahi kuifikisha Al Hilal robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kutwaa CHAN 2016 na DR Congo, na kuiwezesha RS Berkane ya Morocco kuchukua Kombe la Shirikisho mwaka 2020.




