Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Abel Paul, ametoa shukrani za dhati kwa wadau wote wa sekta ya habari kwa ushirikiano wao uliowezesha kukamilika kwa utafiti wake wa kitaaluma.
Kwa namna ya kipekee, amevishukuru vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo Nipashe, pamoja na wanahabari na watumishi wote wa sekta hiyo kwa mchango wao muhimu katika kufanikisha zoezi hilo.
Abel amesema ushirikiano huo ulikuwa nguzo imara katika kufanikisha utafiti wake, hasa kutokana na unyeti wa mada na nafasi kubwa ya sekta ya habari katika jamii.

Ameeleza kuwa utafiti huo ulikuwa sehemu ya mahitaji ya shahada ya uzamili katika masuala ya ulinzi wa taarifa na utawala bora, ambapo alichambua kwa kina usalama wa taarifa, maadili ya taaluma ya habari pamoja na mifumo ya uwazi na uwajibikaji.
Aidha, amesema matokeo ya utafiti wake yamekuja na mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kuboresha uendeshaji na uripoti wa masuala ya kihabari, si tu nchini Tanzania bali pia katika ngazi ya kimataifa.
Amebainisha kuwa utafiti huo umechangia kujibu baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya habari na kutoa dira ya maboresho yenye tija kwa wadau wote.
Akihitimisha, Abel amesisitiza kuwa maarifa na matokeo ya utafiti huo yatatumika kama nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi wa taarifa, kukuza mawasiliano yenye tija na kuendeleza misingi ya utawala bora kwa maendeleo endelevu ya jamii.




