Saturday, March 7, 2026
spot_img
HomeHabariJaji Mkuu Masaju awakemea waajiri wasiosilisha michango ya wafanyakazi Mifuko ya Hifadhi...

Jaji Mkuu Masaju awakemea waajiri wasiosilisha michango ya wafanyakazi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, amekemea vikali tabia ya baadhi ya waajiri nchini kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii, hali inayosababisha kufunguliwa kwa mashauri mengi ya migogoro ya kazi mahakamani.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Tisa wa Kamati ya Utatu, Jaji Masaju alisema ni muhimu waajiri kuthamini maslahi na utu wa wafanyakazi badala ya kujikita kutengeneza faida pekee.

“Mifuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF ipo kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi wanapofikia uzee, wanapopata ulemavu au hata familia zao baada ya kifo. Inasikitisha kuona baadhi ya waajiri wanakata michango ya wafanyakazi lakini hawaiwasilishi, au wanaichelewesha,” alisema.

Jaji Masaju alionya kuwa kitendo hicho ni kosa la kisheria na dhuluma kwa mfanyakazi, akisisitiza waajiri wote kulipa madeni na kuhakikisha michango ya kila mwezi inawasilishwa kwa wakati. Vilevile, aliwataka waajiri ambao bado hawajajisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kufanya hivyo kwa manufaa ya wafanyakazi wao.

Aidha, aliutaka Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) kuongeza ukaguzi na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili kulinda afya na usalama wao kazini.

Kuhusu mashauri ya hifadhi ya jamii, Jaji Masaju alisema anatarajia kurekebisha Kanuni za Uendeshaji wa Sheria ya Madai ili mashauri ya NSSF yasikilizwe na kutolewa uamuzi haraka, bila mlolongo mrefu wa kesi. Pia alishauri mifuko hiyo kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP), kwa kuwa kushindwa kuwasilisha michango kunaweza kutafsiriwa kama kosa la uhujumu uchumi linalosababisha hasara kwa mamlaka husika.

Aliwataka wafanyakazi wa sekta binafsi na serikalini kufanya kazi kwa bidii bila kusukumwa, huku akiwahimiza kutambua na kufuatilia haki zao. “Hifadhi ya jamii ni msingi wa utu. Tuendelee kuwa taifa la haki, linalothamini binadamu kabla ya faida,” alisisitiza.

Pia aliwataka waajiri kutekeleza viwango vya usalama kazini, kutoa mafunzo mara kwa mara, kuwasiliana vizuri na OSHA pamoja na kutoa taarifa za ukiukwaji wa usalama kwa siri na ujasiri.

Katika hotuba yake, Jaji Masaju alimpongeza Mtendaji Mkuu wa OSHA, Justina Mashimba, kwa kuingia makubaliano na Mahakama ya kutoa mafunzo ya miaka miwili kwa maofisa wa mahakama na wadau wake, hatua aliyoeleza kuwa inaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi.

Alimshauri pia kusaidia Mahakama kwa kununua pikipiki kwa mahakimu walioko vijijini, kompyuta mpakato na kujenga mahakama mpya.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Jaji Masaju alisema nguzo yake ya kwanza inahusu uchumi jumuishi na shindani, hivyo ni lazima kuhakikisha makundi kama watu wenye ulemavu yanashirikishwa ipasavyo. Alieleza kuwa mpango wa mafunzo uliopo sasa unajumuisha pia watumishi wenye ulemavu, jambo linaloendana na nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 inayolenga kuimarisha ushirikishwaji wa wadau.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Mchango wa Wadau wa Haki Kazi katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050”. Jaji Masaju alisema kaulimbiu hiyo inalenga kutambua kuwa kazi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya mtu mmoja na taifa kwa ujumla.

Aliishukuru Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kufadhili mafunzo mbalimbali kwa majaji, ikiwemo mafunzo ya hivi karibuni kwa majaji wafawidhi jijini Arusha. Katika hafla hiyo, alizindua juzuu mbili za maamuzi ya Mahakama Kuu kuhusu migogoro ya kazi nchini — ya kwanza ikihusu miaka 2010 hadi 2022, na ya pili ikihusu miaka 2023 hadi 2024.

Katika hitimisho la hafla hiyo, Jaji Mkuu Masaju alikabidhiwa Tuzo Maalum kutambua mchango wake katika kukuza mazungumzo ya kijamii na haki za kazi nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments