Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeutaarifu umma wa Watanzania kuwa kumeibuka watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuchapisha maudhui yenye lengo la kulihusisha Jeshi na masuala ya kisiasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya JWTZ, baadhi ya maudhui hayo yamekuwa yakitolewa na watu walioko katika mazingira ya kijeshi, wanaojinasibisha na Jeshi, pamoja na wale waliowahi kuachishwa kazi kutokana na tabia na mienendo mibaya. Wengine pia wamekuwa wakijihusisha na siasa na uanaharakati huku wakilitumia Jeshi kama kisingizio cha hoja zao.
Jeshi hilo limeeleza kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, likiongozwa na misingi ya uaminifu, utii na uhodari, huku likizingatia kiapo cha ulinzi wa taifa.
JWTZ limewataka Watanzania kuendelea kuwa na imani nalo, kwani litaendelea kusimamia wajibu wake bila kushirikishwa katika masuala ya kisiasa.




