Thursday, March 12, 2026
spot_img
HomeHabariKabisama : Tanzania tunjivunia haki, mshikamano, majadiliano

Kabisama : Tanzania tunjivunia haki, mshikamano, majadiliano

Kiongozi wa asasi za kiraia nchini Tanzania, Martina Kabisama, Mratibu wa Kitaifa wa SAHRiNGON Tanzania Chapter na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Action for Change, ameangazia maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania katika kuimarisha haki za binadamu, mshikamano wa kijamii na majadiliano ya kitaifa katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini Geneva.

Akizungumza katika mjadala uliofanyika ndani ya Palais des Nations, Kabisama aliwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kukuza majadiliano ya kitaifa, mshikamano wa kijamii na heshima kwa haki za binadamu nchini Tanzania. Alieleza kuwa nchi imeendelea kujijengea msingi imara wa amani, umoja na ustahimilivu wa kijamii kwa muda mrefu.

Katika wasilisho lake, alibainisha kuwa Tanzania imeimarisha utawala shirikishi na ushiriki wa wananchi katika maendeleo kupitia dhamana za kikatiba zinazolinda uhuru wa kutoa maoni, kujumuika na kushiriki katika shughuli za kijamii na kitaifa. Hali hiyo imeziwezesha asasi za kiraia kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya uraia, utetezi wa sera, ufuatiliaji wa haki za binadamu na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya kidemokrasia.

Kabisama aliongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha haki za kijamii na kiuchumi kupitia upanuzi wa huduma muhimu za jamii, ikiwemo elimu, afya, maji, makazi na fursa za ajira. Aidha, alibainisha mafanikio katika kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi kupitia mifumo ya kisheria kama Sheria ya Ardhi ya Vijiji na Sheria ya Ardhi, hatua zilizoongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uzalishaji na kuimarisha ustawi wa kaya.

Kwa upande wa vijana, alisisitiza uwekezaji katika elimu, ujuzi, ubunifu na teknolojia kama msingi wa kujenga taifa lenye maendeleo jumuishi na endelevu. Hata hivyo, alitaja changamoto zilizopo, ikiwemo tofauti za maendeleo kati ya maeneo na upatikanaji usio sawa wa baadhi ya huduma za msingi, ambazo zinahitaji juhudi za pamoja kuzikabiliana.

Kabisama pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya asasi za kiraia na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, akieleza kuwa ushirikiano huo ni nyenzo muhimu ya kukuza uwajibikaji, kupanua upatikanaji wa haki na kulinda maslahi ya makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Aidha, alitaja mchango wa asasi za kiraia katika utekelezaji wa programu mbalimbali za elimu ya uraia, msaada wa kisheria na ufuatiliaji wa haki za binadamu, jambo lililosaidia wananchi kutambua haki zao na kushiriki ipasavyo katika maendeleo ya jamii na taifa. Alirejelea Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kama hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma za haki kwa wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji maalum.

Katika hitimisho la wasilisho lake, Bi. Kabisama alisisitiza kuwa heshima kwa utu wa binadamu lazima iendelee kuwa msingi wa maendeleo endelevu, amani ya kijamii na mshikamano wa taifa. Alieleza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kutenganishwa na majadiliano ya wazi, taasisi imara na ushiriki jumuishi wa wananchi.

Aidha, alinukuu mwelekeo wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, unaojengwa kwenye misingi ya 4Rs: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya, akieleza kuwa mfumo huo unaendelea kutoa nafasi kwa Tanzania kuimarisha utawala bora, mshikamano wa kitaifa na mageuzi yanayogusa wananchi kwa upana.

Ushiriki wa Kabisama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaakisi nafasi inayozidi kuimarika ya asasi za kiraia za Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, pamoja na dhamira ya nchi kuendelea kukuza haki za binadamu, majadiliano ya kitaifa na maendeleo jumuishi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments