Sunday, March 15, 2026
spot_img
HomeGeneral News‎Kamati Bunge yasisitiza udhibiti upotevu wa maji

‎Kamati Bunge yasisitiza udhibiti upotevu wa maji

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha huduma za maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, sambamba na kuongeza juhudi za kudhibiti upotevu wa maji katika mfumo wa usambazaji.


‎Wito huo umetolewa baada ya kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa ya utendaji ya DAWASA katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.

‎Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Masanja Kadogosa, amesema eneo la huduma la DAWASA linaendelea kukua kwa kasi kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi na makazi ya wananchi.


‎ Kutokana na hali hiyo, amesema ni muhimu mamlaka hiyo kuhakikisha inakamilisha miradi ya maji inayoendelea pamoja na kubuni vyanzo vipya vitakavyosaidia kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Kadogosa amesisitiza kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na uchumi nchini pamoja na kuwa lango kuu la biashara kwa mataifa mengi, huku Mkoa wa Pwani ukiendelea kukua kwa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa wa viwanda.

‎Amesema maeneo hayo yanahitaji mikakati madhubuti ya usimamizi wa huduma za maji ili kukidhi mahitaji ya wananchi na shughuli za uzalishaji.

‎ “Mkoa wa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na uchumi na pia ni lango la biashara kwa mataifa mengi. Vilevile Mkoa wa Pwani ni eneo muhimu la viwanda. Hivyo ni lazima kuwepo mikakati madhubuti ya usimamizi wa huduma za maji ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye,” amesema Kadogosa.

‎Aidha, ameielekeza DAWASA kuhakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maji pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya upotevu wa maji kwenye miundombinu ya usambazaji.

‎Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa mamlaka hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi wa Mipango, Tafiti na Ufuatiliaji wa DAWASA, Paul Sulley, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kimkakati yenye lengo la kuboresha huduma za maji katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani.

‎Sulley ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa Maji wa Bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini, ununuzi wa pampu kubwa kwa ajili ya visima virefu vya Kimbiji, pamoja na maandalizi ya mradi wa kutoa maji katika Mto Rufiji.

‎Amesema utekelezaji wa miradi hiyo kwa pamoja unatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa maji na hivyo kuimarisha uhakika wa huduma kwa wakazi wa mikoa hiyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments