Kampuni ya Sukari ya Kilombero, kupitia chapa yake maarufu ya bidhaa Bwana Sukari, imewataka wasambazaji na washirika wa kibiashara kuchangamkia fursa zinazotokana na Mradi wa Upanuzi wa K4, ambao uko katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kazi rasmi.

Akizungumza kwenye maonesho hayo, Fimbo Butallah, Mkurugenzi wa Biashara na Ugavi wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kukuza soko:
“Kampuni ya Sukari ya Kilombero, kupitia bidhaa yetu ya Bwana Sukari, tumejipanga kikamilifu kuhudumia soko. Mradi wa Upanuzi wa K4, ambao sasa uko karibu kuanza kazi, utaongeza mara mbili uwezo wetu wa uzalishaji—tutaongeza tani 144,000 kwa mwaka, na hivyo kupeleka jumla ya uzalishaji kutoka tani 126,000 hadi tani 271,000 kwa mwaka.”
Butallah aliongeza kwa kueleza fursa zitakazotokana na mradi huu kwa washirika wa kibiashara:
“Upanuzi huu unamaanisha fursa kubwa kwa wasambazaji na washirika. Kwa uzalishaji kuongezeka mara mbili, tutapanua mtandao wa usambazaji, kuunda ajira zaidi, na kuleta manufaa chanya katika mnyororo mzima wa thamani wa Bwana Sukari.”


Akiwakilisha wakulima wa Bonde la Kilombero, Clemency Stephen Mjami kutoka Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Miwa Mkula (Mkula Cane Growers AMCOS) alieleza matumaini yake:
“Kama mkulima, nina imani kubwa na Mradi wa Upanuzi wa K4. Hivi sasa tunasambaza tani 600,000 za miwa kwenye kiwanda. Baada ya kukamilika, tunatarajia kufikisha hadi tani 1,500,000, jambo litakaloongeza kwa kiwango kikubwa ushiriki wa wakulima.”
Mjami pia alisifu mfumo wa malipo wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero kwa uwazi na kwa wakati, unaosaidia wakulima kupata huduma za kifedha na elimu ya masuala ya fedha:
“Mfumo wa malipo wa Kilombero Sugar unajenga imani na taasisi za kifedha, na hivyo kuwawezesha wakulima kupata mikopo na huduma za kifedha kwa ujasiri.”


Katika banda la Bodi ya Sukari, Prof. Kenneth Bengesi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, aliipongeza Kampuni ya Sukari ya Kilombero kwa uwekezaji wake wa kimkakati:
“Tunapongeza Kampuni ya Sukari ya Kilombero kwa uwekezaji wa kimaono wa zaidi ya shilingi bilioni 744 katika kupanua viwanda vyake vya sukari. Serikali itaendelea kujitahidi kulinda sekta ya sukari ili kuhakikisha upatikanaji wa sukari wa kutosha kitaifa na ustahimilivu wa muda mrefu.”
Kadri Maonesho ya Nane Nane yanapofikia kilele chake, yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha teknolojia za kisasa za kilimo, kuimarisha ushirikiano wa sekta, na kufungua fursa mpya kwa wadau katika mnyororo wa thamani.



