Beki wa Simba SC, Shomari Salum Kapombe, ametolewa kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka anayecheza katika klabu za Afrika, baada ya kupitwa na nyota wengine watatu walioteuliwa kuingia hatua inayofuata.
Kapombe amezidiwa kete na beki wa kulia raia wa Morocco, Mohamed Chibi, pamoja na washambuliaji wawili: Mkongo Fiston Mayele wa Pyramids FC ya Misri na Mmorocco Oussama Lamlioui wa RS Berkane, ambao sasa wanaendelea kuwania tuzo hiyo.
Awali, wachezaji wengine sita waliokuwa katika orodha ya mchujo ni Ismael Belkacemi (Algeria/Al Ahli Tripoli), Blati Touré (Burkina Faso/Pyramids FC), Issoufou Dayo (Burkina Faso/RS Berkane), Ahmed Samy (Egypt/Pyramids), Emam Ashour (Egypt/Al Ahly), Ibrahim Adel (Egypt/Pyramids) na Mohamed Hrimat (Morocco/AS FAR).
Katika upande wa klabu, Simba SC pia imetolewa kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka ya CAF, ambapo Pyramids ya Misri, RS Berkane ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ndizo zilizofanikiwa kuingia fainali. Simba ilikuwa miongoni mwa timu 10 zilizoingia awali kwenye mchujo, ikiwemo CR Belouizdad na CS Constantine za Algeria, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Orlando Pirates na Stellenbosch za Afrika Kusini, pamoja na Al Hilal ya Sudan.
Wakati huohuo, mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Francis Mzize, ameingizwa kwenye orodha ya awali ya Tuzo ya Bao Bora Afrika kupitia bao lake alilofunga katika ushindi wa 3-1 dhidi ya TP Mazembe Januari 4 mwaka huu, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Mzize alifunga mabao mawili, na bao linalowania tuzo ni lile la dakika ya 33 lililosawazisha, baada ya TP Mazembe kutangulia kupata bao dakika ya 16 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na kipa wa Senegal, Aliouane Badara Faty.
Mzize pia alifunga bao la tatu dakika ya 60, huku kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki (ambaye sasa yuko Wydad Athletic ya Morocco), akifunga bao la pili dakika ya 56.




