Selemani Mwalimu, straika mpya wa Simba akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, ni miongoni mwa wachezaji 23 walioitwa kuunda kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya michezo miwili ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Niger (Septemba 9) na Jamhuri ya Congo (Septemba 5).

Nahodha Mbwana Samata, Charles M’mombwa, Simon Msuva na Dismas Novatus pia wako kwenye kikosi hicho kilichotarajiwa kuingia kambini kesho. Kocha Mkuu, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amemuacha kipa Aishi Manula aliyejiunga na Azam FC. Kikosi hiki kimeundwa kwa asilimia kubwa kutoka kwenye kikosi kilichoshiriki CHAN Kenya, kilichoibuka bingwa.
Miongoni mwa wachezaji waliotajwa ni Yacoub, Hussein Masalanga (Singida Black Stars), Antony Remmy (Azam), Shomari Kapombe, Yusuph Kagoma, Wilson Nangu, Lucas Mwaikenda, Pascal Msindo, Yahya Zaid, Abdul Selemani Sopu, Feisal Salum, Idd Selemani ‘Nado’, Mohamed Hussein, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Dismas (Goztepe FC, Uturuki), M’mombwa (Floriana FC, Malta), Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), na Msuva (Al Talaba SC, Iraq).
Tanzania ipo Kundi E, ikiwa nafasi ya pili kwa pointi tisa, nyuma ya Morocco yenye pointi 15, ikijaribu kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani Marekani, Canada na Mexico.




