Thursday, December 11, 2025
spot_img
HomeBiasharaKilombero Sugar yatoa wito Wakulima wa Miwa kuchangamkia fursa mradi upanuzi Kiwanda...

Kilombero Sugar yatoa wito Wakulima wa Miwa kuchangamkia fursa mradi upanuzi Kiwanda cha K4 

Kampuni ya Sukari Kilombero imetoa wito kwa wakulima wa miwa wa Bonde la Kilombero kuchangamkia fursa zinazotokana na Mradi wa Upanuzi wa K4, ambao sasa uko katika hatua za mwisho kabla ya kuanza rasmi.

Wito huu umetolewa wakati wa Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane yaliyofanyika mkoani Morogoro, ambapo Kilombero Sugar imeshiriki kimkakati kuonyesha maendeleo ya mradi huu wa mageuzi.

Mwaka huu, Kilombero Sugar imeshiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Tanzania yanayofahamika kwa jina maarufu la Nane Nane, katika ngazi ya Taifa jijini Dodoma na Kanda ya Mashariki mjini Morogoro. Lengo kuu la ushiriki wa kampuni ni kuonesha mafanikio ya Mradi wa K4 pamoja na kutangaza chapa yake maarufu , Bwana Sukari.

Akizungumza wakati wa maonyesho hayo, Derick Stanley, Mkurugenzi wa Mahusiano na mawasiliano  ya Kampuni wa Kilombero Sugar amesema:

 “Ushiriki wetu kwenye maonyesho ya Nane Nane 2025 unalenga kuonyesha fursa kubwa zilizopo kupitia uwekezaji wetu wa kimkakati katika Mradi wa Upanuzi wa K4. Kilombero Sugar imewekeza zaidi ya TZS bilioni 744 katika mradi huu. Tunatarajia kuona ongezeko la ununuzi wa miwa kutoka tani 600,000 hadi tani 1,500,000 kwa mwaka, jambo litakaloongeza mapato ya wakulima hadi kufikia takriban TZS bilioni 170 ifikapo mwaka 2030.”

Bw. Stanley amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii, akiwahimiza wakulima na wakazi wa Bonde la Kilombero kuchangamkia fursa hizo ipasavyo. Idadi ya wakulima waliosajiliwa inatarajiwa kuongezeka kutoka wakulima  8,000 wa sasa na kufikia kati ya 14,000 hadi 16,000,  hatua itakayochochea ajira binafsi na fursa zaidi za ajira katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Akizungumza katika banda la Kilombero Sugar, Prof. Kenneth Bengesi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wake wa kimkakati katika kiwanda kipya cha kisasa cha K4:

 “Tunaipongeza Kilombero Sugar kwa maono haya makubwa. Kiwanda hiki kipya chenye teknolojia ya kisasa kitabadilisha taswira ya sekta ya sukari nchini. Kitazidisha mara mbili uwezo wa uzalishaji wa kampuni, kuongeza tani 144,000 za sukari kwa mwaka, na kupandisha uzalishaji kutoka tani 126,000 hadi 271,000 kwa mwaka.”

Kwa upande wake, Kennedy Charles Rwehumbiza, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania (TSPA), amesisitiza kuwa wadau wa sekta hiyo wanapaswa kujivunia uwekezaji huu wa kimkakati. Ametoa wito kwa serikali kuendeleza na kulinda miradi ya mageuzi kama K4 ambayo ni nguzo ya ustawi wa sekta ya sukari nchini Tanzania.

Victor Byemelwa, Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano na Wadau wa Kilombero Sugar na msimamizi wa ushiriki wa maonyesho haya kwa upande wa Morogoro na Dodoma, ameongeza:

 “Mwaka huu tumeshiriki kwa mafanikio makubwa katika maonesho ya kitaifa Dodoma na Kanda ya Mashariki Morogoro. Tumepokea maoni chanya kutoka kwa wageni waliotembelea banda letu, wengi wakivutiwa na ubora na utofauti wa bidhaa za Bwana Sukari pamoja na dhamira yetu ya kujenga thamani ya pamoja.”

Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa ajili ya kuonesha teknolojia za kisasa, kuunganisha wadau wa sekta ya kilimo, na kutambua fursa za uwekezaji katika sekta hii inayokua kwa kasi nchini Tanzania.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments