Kocha Mkuu wa Bunda Queens, Alley Ibrahim, amesema timu yake ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Simba Queens kutokana na kukosa wachezaji muhimu.
Amesema wachezaji 11 hawakusafiri baada ya kubaki Mara kufanya mtihani wa kidato cha nne, huku wengine saba wakikosa leseni.
Amesema kipindi cha kwanza walicheza vizuri, lakini katika kipindi cha pili uwezo uliwashuka na kulazimika kutumia kikosi cha pili kwa mfumo wa kujilinda ili kuepuka mabao mengi. Pia aliisifu Simba Queens kwa ubora wao.
Kocha msaidizi wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alisema walikabiliana na timu ngumu na kufanya maboresho kipindi cha pili yaliyowapa matokeo.
Alisema lengo lao ni kutwaa ubingwa msimu huu. Ushindi huo umeiweka Simba kileleni na pointi 6, huku Jentrix Shikangwa akiendelea kuongoza ufungaji kwa mabao manne.




