CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepasuka rasmi baada ya Makamu Mwenyekiti wake Tundu Lissu, kutangaza nia ya kugombea uenyekiti unaoshikiliwa na Freeman Mbowe, aliyedumu kwenye kiti hicho kwa miaka 20.

Awali Lissu alitangaza kutetea nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti, lakini amebadilisha mtazamo wake, badala yake akamuandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akimuarifu uamuzi wake wa kuitaka nafasi ya juu kabisa katika chama hiki cha upinzani.
Uamuzi wa Lissu kuitaka nafasi hiyo imetajwa kama sehemu ya kuendeleza joto na mpasuko kutokana na baadhi ya wadau wa chama hicho kuamini ni Mbowe tu anayeweza kushikilia kiti cha Mwenyekiti wa Chadema.
“Mzee Edwin Mtei na Mzee Bob Makani hawakutaka kukaa madarakani mpaka watakapolazimishwa kuondoka kwa aibu. Waliandaa utaratibu wa kuondoka madarakani kwa hiari yao,” Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema.
Maneno ya Lissu kuhusu viongozi kungángánia madaraka ni kama kejeli kwa Mwenyekiti wake Mbowe, aliyeshikilia nafasi hiyo kwa miaka 20 huku kila anayetangaza nia ya kuitaka nafasi hiyo kutimuliwa kwenye chama hicho.