SHIRIKA la Uwezeshaji wa Kisheria linalofahamika kama Legal Service Facilities(LSF), kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwamo Smile for Community, wamechangia kuboresha miundombinu ya shule ya Sekondari ya Nanyamba na Mnyawi zilizopo mkoani Mtwara.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Run for Binti, Flora Njelekela amesema maboresho waliyofanya kwenye shule hizo ni ujenzi wa vyoo vyenye matundu 12 kila shule ambavyo wamevijenga kupitia programu ya Run for Binti Marathon awamu ya tatu.
“Msimu wa pili na wa tatu wa mbio hizi umekuwa wa mafanikio kwa kufikia jamii ya mkoa wa Mtwara hususani shuleni, tunaamini kwamba kupitia hii jamii itazidi kusaidika,”amesema Flora.
Mbali na kujenga choo, amesema wametoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule hiyo pamoja na kuoanda miti.
Amesema wamekuwa wakiendesha marathoni hizo kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule.
“Lengo letu ni kuboresha mazingira ya elimu na afya kwa wanafunzi wa kike na kiume wanaosoma katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa nchi.
“Tunawapatia pia mabinti wa shule, taulo za kike ambazo zinaweza kutumika zaidi ya mara moja tukilenga kuimarisha afya na usafi wa wanafunzi hao wa kike,”amesema Flora.
Kadhalika, alisema wamekuwa wakiwapatia elimu ya ukatili wa kijinsia, elimu ya fedha , hedhi salama na afya ya uzazi , utunzaji wa mazingira, kupanda miti pamoja na mafunzo kuhusu nishati.


” Pia tulifanya kazi ya utoaji wa elimu muhimu kwa wanafunzi na jamii ya Mtwara kupitia wadau mbalimbali wakiwamo Stanbic Bank Tanzania, Marie Stopes Tanzania, na Girl Guide Tanzania juu ya masuala ya usafi,”amesema Frola.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewashukuru wadau kwa kufanikisha miradi hiyo na kupongeza juhudi zinazofanywa na wadau katika kutatua
changamoto za jamii ikiwamo wakazi wa mkoa wa Mtwara.
“Nawashukuru sana wadau kwa kuchagua Mtwara kama sehemu ya kutekeleza miradi hii muhimu.


“Maboresho haya yatanufaisha wanafunzi na jamii nzima ya Mtwara. Tunawakaribisha kuendelea kuwekeza katika miradi mingine ya maendeleo, niihamasishe jamii kutumia fulsa hii vizuri na mafunzo waliyoyapata yakasaidie kupunguza changamoto zilipo hususani za ndoa na kuwalinda wanawake,”amesema Mwaipaya.

