Lucy Antony Michael (35), mkazi wa Yombo Dovya, Mtaa wa Makangarawe, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, amedai kuvamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa anatoka nyumbani kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Lucy amesema watu hao walimvamia ghafla na kumpiga, wakimsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake. Amesema anaamini tukio hilo linahusiana moja kwa moja na maandamano yaliyofanyika siku chache zilizopita, ambapo baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki walitembea hadi Ubalozi wa Vatican uliopo hapa nchini.
Kwa mujibu wa Lucy, wakati wa shambulio hilo, watu waliomvamia walimtuhumu kwa madai ya kujifanya msemaji wa Serikali na kumuuliza ni kwa mamlaka gani alishiriki kwenda katika Ubalozi wa Vatican.
“Jambo kubwa walilokuwa wakidai ni kuniambia kuwa najifanya msemaji wa Serikali, chawa, na kuniuliza nina mamlaka gani ya kwenda Ubalozi wa Vatican,” amesema Lucy akinukuu maneno aliyodai kuambiwa na washambuliaji wake.
Lucy ni miongoni mwa waumini wa Kanisa Katoliki waliojitambulisha hadharani kuwa walishiriki kufika katika Ubalozi wa Vatican siku chache zilizopita, ambapo walikabidhi barua ya malalamiko wakilalamikia mwenendo wa baadhi ya viongozi wa Kanisa hilo.
Tukio hilo limeibua maswali na wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusu usalama wa raia wanaotoa maoni au kushiriki katika masuala yanayohusu taasisi za kidini na kijamii, huku Lucy akitoa wito kwa vyombo vya dola kuchunguza kwa kina tukio hilo na kuwachukulia hatua wahusika.




