Madaktari bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan, wakiwamo wa watoto, wanawake, uzazi na magonjwa ya ndani, wameanza kambi ya matibabu mkoani Lindi; ikiwa ni awamu ya nne ya mpango wa serikali kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi.
Mabingwa hao waliwasili mkoani humo jana na kupokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Zuwena Omari, ambaye alisema kambi hiyo inawapa wananchi ahueni kwa kuwaepusha kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa.
“Zoezi hili ni zuri kulingana na uwekezaji wake, uwepo wake unasaidia wananchi kupata huduma katika maeneo yao ya karibu. Wito wangu tuendelee kutumia fursa hii, na kila mwenye changamoto afike katika vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema Zuwena.
Taarifa ya Wizara ya Afya, imesema kwamba jumla ya wataalam mabingwa 47 watatoa huduma katika kambi hiyo, wakiwemo wa magonjwa ya ndani, usingizi, upasuaji, meno, watoto, pamoja na wanawake na uzazi, ambao watatoa huduma katika halmashauri zote saba za mkoa wa Lindi.
Kambi hiyo inalenga kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.




