Thursday, December 18, 2025
spot_img
HomeAfyaMadaktari Bingwa 55 wa Dk. Samia waweka kambi Mtwara

Madaktari Bingwa 55 wa Dk. Samia waweka kambi Mtwara

Na WAF, Mtwara

Huduma za matibabu ya kibingwa kupitia kambi maalum ya Madaktari Bingwa na wataalam wabobezi wa afya wapata 55 wa Dk. Samia zimeanza rasmi kutolewa kwa wananchi mkoani Mtwara kuanzia Septemba 15 hadi 19, 2025 kwa Halmashauri zote tisa (9) za mkoa huo.

Hayo yamesemwa Septemba 15 , 2025 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dk. Benedicto Ngaiza wakati wa mapokezi ya madaktari hao ambao watatoa huduma za kibingwa na bobezi za magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto na watoto wachanga, upasuaji, ganzi salama na magonjwa ya ndani.

Dk. Ngaiza amesema katika awamu tatu zilizopita madaktari bingwa wa Dkt. Samia wamewahudumia jumla ya wagonjwa 8,682 na kwa awamu hii ya nne zaidi ya wananchi 2,800 wanatarajiwa kunufaika na ujio wa madaktari hao katika hospitali za halmashauri zao.

Pia Dk. Ngaiza amesema ujio huo ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo kupata huduma bora karibu yao na watumishi kwenye vituo vya afya ngazi ya msingi kupata kujifunza utaalam mbalimbali wa kibingwa kutoka kwa madaktari hao.

“Serikali imewekeza miundombinu na vifaa tiba vya kisasa katika hospitali zetu tunaamini kwa kipindi hiki kifupi itakuwa ni fursa kwa wataalam wetu wa afya kujifunza kutoka kwa mabingwa hawa namna ya kutumia vifaa hivyo,” amesema Dk. Ngaiza

Kwa upande wake Mratibu kutoka Wizara ya Afya Edith Senga amesema lengo la ujio wa madaktari bingwa hao ni kusogeza huduma kwa wananchi, kuongeza uwezo kwa wataalam katika ngazi za afya za msingi na kuainisha wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa na bobezi kwa ajili ya kupata rufaa za juu zaidi.

“Wizara ya Afya inashirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI katika kuendesha zoezi hili ambapo Halmashauri zote 9 za mkoa wa mtwara zitafikiwa kwa kupata madaktari bingwa na bobezi kwa seti,” amesema Senga.

Aidha Senga ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Mtwara kujitokeza kwa wingi katika hospitali za halmashauri zao ili kupata huduma za kibingwa na bobezi karibu yao kwa muda uliowekwa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments