Madaktari wa Tanzania wahitimisha kambi tiba Comoro kwa ufanisi mkubwa

MADAKTARI wa Tanzania wamerejea nchini baada ya kuhitimisha Kambi tiba nchini Comoro kwa kutoa huduma kwa wagonjwa 2,770 na kufanya upasuaji kwa wagonjwa saba.

Kwenye kambi hiyo ya siku saba wameweza kubaini wagonjwa takriban 269 wanahitaji rufaa za matibabu zaidi nje ya nchi na pia kuainisha fursa zaidi za ushirikiano katika sekta ya Afya.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam mara baada kuwasili katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge alisema kambi imekwenda vizuri na wamefanikiwa kuwahudumia watu wengi.

Alisema nje ya kambi hiyo walifanya kikao maalum na Waziri wa Ulinzi wa Comoro ambaye pia ni Msaidizi wa Rais na Katibu Mkuu wa Chama tawala kinachoongoza Jamhuri ya Comoro.

“Kwenye vikao kama saba tulivyofanya tulijadili fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano kwenye sekta ya afya baina ya Tanzania na Comoro na yeye Msaidizi wa Rais wa Comoro kwenye kikao aliongelea fursa kama watapatikana madaktari wa Tanzania kufanyakazi Comoro,” alisema Dk Kisenge na kuonegeza

“Nje ya kambi tuliangalia uwezekano wa hospitali ya Tanzania kuchukua kazi za hospitali moja ya Comoro yenye vitanda 100 na kuangalia uwezekano wa kuangalia utaalamu ambao haupatikani Comoro sisi watanzania tuupeleke kwao,” alisema

“Tumefanya vikao mbalimbali vyenye tija, tumekaa na Waziri wa Afya wa Comoro na tumekaa na Mshauri Mkuu wa Rais wa Comoro kuangalia mambo ya msingi ambayo tunaweza kushirikiana na uwekezaji ambao umefanyika Tanzania,” alisema

“Tulikaa na Jumuiya inayojihusisha na elimu ya saratani tulikaaa na Mkuu wa idara ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Comoro tukachambua kozi za afya ambazo wanazitoa kwenye vyuo vyao na ambazo hazitolewe kwao lakini Tanzania zipo ili tuweze kuzipeleka,” alisema

Dk Kisenge alisema vikao hivyo vilihudhuliwa na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Said Yakub, Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Aisha Mahita na Mkurugenzi wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel.

Dk. Kisenge aliishukuru Global Medicare ambayo ilikuwa mratibu mkuu wa kambi hiyo kwa mafanikio yaliyopatikana na aliwashukuru madaktari walioshiriki kwenye kambi hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na kuweka jina kubwa nchini Comoro kwenye kambi hiyo.

Dk Kisenge alisema kuwa kambi iliyomalizika Comoro imekutanisha wadau mbalimbali na kufanya vikao vitakavyoleta tija kwenye ushirikiano wa sekta ya afya Comoro na Dar es Salaam.

“Kwa uwekezaji tulionao kwenye hospitali zetu ili nchi zinazotuzunguka zinufaike na uwekezaji huo lazima tumuunge mkono Rais wetu kwa kufanya kama Comoro na Global Medicare isichoke kuratibu kambi kama hizo kwasababu tunataka kupiga hatua nyingine na madaktari wote nchini wawe tayari inapotokea kambi kama hii wawe tayari kwenda kama walivyofanya Comoro,” alisema

Naye Mkurugenzi wa Globalmedicare, Abdulmalik Mollel alishukuru ubalozi wa Tanzania nchini Comoro na Mkurugenzi wa JKCI, Dk Kisenge kwa kumwamini na kumpa fursa ya kuratibu kambi ya matibabu hayo.

Alimshukuru Dk Kisenge wa JKCI na wakurugenzi wa hospitali za Benjamin Mkapa, MOI, Ocean Road na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa kukubali kutoa madaktari na wataalamu wao kushiriki kwenye kambi hiyo.

Alimshukuru pia Profesa Mohamed Janabi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Utalii Tiba kwa ushirikiano aliouonyesha wa kupeleka wataalamu wake nchini Comoro kuendesha kambi hiyo.

Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya, Aisha Mahita alishukuru Wizara ya Afya kwa kuridhia yeye kwenda Comoro ambapo ameona halihalisi ya uhitaji mkubwa wa madaktari wa Tanzania nchini Comoro.ahita ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuridhia yeye kwenda Comoro ambapo ameona halihalisi ya uhitaji mkubwa wa madaktari wa Tanzania nchini Comoro.

Ameishukuru Global Medicare kwa kuratibu kambi hiyo kwa ufanisi mkubwa  na kuongeza kuwa kwamba wamegundua kuwa afya ni uchumi na tiba ni talii  na ni fursa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *