Madawati 300 yatolewa na Lions Club Infinity kuboresha Shule ya Msingi Mbagala

Shule ya Msingi Mbagala imepokea msaada wa madawati 300 kutoka kwa wanachama wa Lions Club Infinity Dar es Salaam, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi shuleni hapo.

Msaada huo umetolewa baada ya wanachama wa klabu hiyo kutembelea shule hiyo mwaka jana, ambapo walitoa msaada wa taulo za kike na kushuhudia changamoto ya baadhi ya wanafunzi kukaa chini kwa kukosa madawati.

“Tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kwa jamii. Hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya kuwasaidia wananchi wake katika sekta mbalimbali. Leo tuko hapa Shule ya Msingi Mbagala kuunga mkono sekta ya elimu kwa kutoa madawati 300,” alisema Shafiya Dosaji, mwanachama wa Lions Club Infinity Dar es Salaam.

Akipokea msaada huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika, aliwashukuru wanachama hao kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha sekta ya elimu na kuunga mkono utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kusaidia wananchi kupitia miradi mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbagala, Simon Omar, aliwashukuru wanachama wa Lions Club Infinity kwa msaada huo muhimu lakini pia aliwataka wadau wengine kuunga mkono shule hiyo kutokana na changamoto nyingine zinazowakabili.

“Shule hii inakabiliwa na changamoto za miundombinu kwani ilijengwa tangu mwaka 1982. Paa lake liko chini, na wakati wa mchana kuna joto kali linalosababisha mazingira magumu ya kusoma. Tunahitaji kupandisha paa hilo. Pia tunahitaji meza za walimu na vifaa vya TEHAMA,” alisema Mwalimu Simon.

Wanachama wa Lions Club Infinity wamesisitiza dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na jamii kwa kutoa misaada mbalimbali inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika sekta za elimu, afya, na ustawi wa jamii.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *