Magereza Singida kuunga mkono Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia

Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Singida wameahidi kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na kuokoa afya za wananchi.

Ahadi hiyo imetolewa leo Agosti 10, 2025, wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kilo 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 395 kwa watumishi wa jeshi hilo. Hafla hiyo imeongozwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Sophia Mgonja, akiwa ameambatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Wakili Mwantumu Sultan.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida, ACP Felix Mwakyusa alimshukuru Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zilizowezesha kufungiwa nishati safi ya kupikia katika magereza.

“Kwa sasa hatutumii tena kuni, na sasa Rais ameona pia atukumbuke sisi watumishi. Tunashukuru sana na tunaahidi kuwa mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayotuzunguka,” alisema ACP Mwakyusa.

Kwa upande wake, Mhandisi Mgonja aliwataka askari wa magereza kuwa mabalozi wa kampeni hiyo kwa ndugu, jamaa na jamii, akisisitiza kuwa nishati safi ya kupikia inalinda afya na mazingira.

“Tunakabiliwa na changamoto za kimazingira kama ukame na upungufu wa mvua kutokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni. Kupitia nishati safi ya kupikia, tutasaidia kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Mgonja.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya, alisema ugawaji wa majiko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mtaalam wa Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali, alisema jumla ya mitungi ya gesi ya kilo 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 395 yanatarajiwa kugawiwa kwa watumishi wa Magereza Mkoa wa Singida.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *