Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewapongeza vijana wanaojiajiri kwa kufuga samaki kwa kutumia vizimba na kutaka wengine waige mfano huo.

Ametoa pongezi kwa vijana hao leo alipotembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB na kukuta simumizi za vijana hao ambao wameweza kufuga samaki na kuingiza faida ya mamilioni.
Majaliwa amesema vijana hao wanatakiwa kushikwa mkono ili waweze kusonga mbele kwa kuwa na mtaji mkubwa utakaowawezesha kuuza samaki kwenye soko la kimataifa.
Amesema vijana hao watumike kama mfano kwa vijana wengine kuingia kwenye ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili waondokane na umaskini kwa kujiajiri wenyewe kama vijana hao wa VIJANA NGUVU KAZI MWANZA.
Naye Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Uhusiano wa Taasisi Mkani Waziri, amemweleza Waziri Mkuu kuwa mradi huo ulizinduliwa mwaka jana na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amemweleza kuwa kupitia mradi huo, vijana wamekopeshwa shilingi milioni 137 ukiwa ni mkopo usio na riba ambapo wamekuwa wakifuga samaki kwenye visimba na kuvuna kila baada ya miezi sita.


Waziri amesema Rais Samia aliipa benki hiyo fedha za kuwakopesha vijana bila riba ili wafanye biashara ya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba .
Ameongeza kuwa mwaka 2018 TADB ilianzisha Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS), ambao umekuwa ukiwasaidia wakulima kupata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha.

Amesema walengwa wa mfuko huo ni nwakulima wadogo, wafugaji, wavuvi, vyama vya ushirika, vikundi vya wakulima, wafugaji na wavuvi, viwanda vidogo na vya kati.
Amesema mnyororo wa thamani unaohusika kwenye eneo hilo ni uzalishaji, usambazaji, usindikaji, usafirishaji na masoko.
“Kiwango cha mkopo kwenye mfuko huu ni kulingana na uhitaji wa mradi husika na tathmini ya benki au taasisi ya kifedha ambayo ni mshirika wa TADB, vigezo na masharti ya mkopo ni baada ya tathmini ya mradi baina ya mkopaji na benki au taasisi ya kifedha shirika,” amesema

