Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, amewakaribisha wanachama wa CHADEMA ambao hawajaridhishwa na mwenendo wa chama hicho, akisisitiza kuwa ACT Wazalendo ni kimbilio la wahanga wa demokrasia.

Katika ujumbe wake, Mchinjita alianzisha kwa kuwatakia heri wanachama wa CHADEMA kwenye uchaguzi wao wa viongozi wa juu unaofanyika leo. amesema:
“Ninawatakia kila la kheri chama cha Demokrasia na Maendeleo @ChademaTz katika mkutano wao mkuu leo. Mkutano huu ni muhimu kwa ustawi wa chama hicho na mwenendo wa demokrasia nchini.”
Aidha, ameeleza kuwa amekuwa akifuatilia kwa karibu hali inayoendelea ndani ya CHADEMA, hasa mivutano ya kisiasa inayohusisha kambi kuu zinazowania nafasi za uongozi.
“Mwenendo wa minyukano ya kisiasa miongoni mwa kambi kuu zinazowania nafasi ya kuongoza chama hicho unaweka rehani uwezo wa kufanya kazi pamoja baada ya uchaguzi,” ameandika Mchinjita.
Akiweka wazi msimamo wa ACT Wazalendo, ameongeza:
“@ACTwazalendo imekuwa kimbilio mara zote kwa wahanga wa demokrasia. Tunawakaribisha wale wote wanaoona safari yao ya kidemokrasia inahitaji jukwaa jipya. Karibuni @ACTwazalendo yenye tunu ya uongozi wa pamoja, uwazi na mijadala ya masuala.”
Uchaguzi wa nafasi za juu za uongozi ndani ya CHADEMA umevuta hisia za wengi, hasa baada ya Tundu Lissu kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho. Uchaguzi huu unachukuliwa kama hatua muhimu katika mustakabali wa CHADEMA na demokrasia kwa ujumla nchini Tanzania.