Makamu wa Rais kushiriki Tigo Z’bar Marathon 2024

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, anatarajiwa kushiriki mbio za Tigo Zanzibar Marathon 2024, zitakazofanyika mwezi ujao visiwani humo.

Aidha, amepongeza waandaaji wa mbio hizo ambazo amezitaja zinaunganisha watu.

“Binafsi napenda sana kushiriki katika mbio hizi, zinawaleta watu pamoja na kushiriki katika kujenga afya, nawapongeza sana waandaaji na wadhamini wa mbio hizi,” alisema.

Alisema mbio hizo ziendelee kuwa endelevu na kuboreshwa zaidi kila mwaka, ili ziwavutie watu wengi zaidi.

“Mungu akitupa uhai na uzima safari hii na mimi nitashiriki, nilikuwa sijawahi kushiriki kwa sababu mbalimbali, napata mwaliko, lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu, sikupata nafasi, mwaka huu nitashiriki,” alisema.

Akizungumzia mbio hizo, mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Tigo Zantel Kanda ya Zanzibar, Azizi Said Ali, alisema maandalizi yanaendelea vizuri na tayari watu wameanza kujiandikisha kwenye vituo mbalimbali, Dar es Salaam na visiwani humo.

Alisema mwitikio umekuwa mkubwa na wanaamini idadi itaongezeka kwa watu kushiriki zaidi katika msimu huu wa tatu wa Tigo Zanzibar Marathon.

“Tunaendelea na maandalizi, na kwa kweli yanaenda vizuri sana, tunatarajia wanariadha na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuja kushiriki,” alisema Ali.

Alisema kwa mwaka huu mbio hizo zitakuwa kuanzia kilometa tano, 10 na kilometa 21 (nusu marathon)

Mbio hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya Tigo, zinafanyika kwa msimu wa tatu mfululizo.

Chanzo: Nipashe

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *