Klabu ya Mtibwa Sugar imeeleza kuwa imepokea wasifu kutoka kwa makocha mbalimbali wa ndani na nje ya nchi waliotuma maombi ya kukinoa kikosi hicho kwa msimu ujao wa Ligi Kuu.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, amesema mchakato wa kutafuta kocha unaendelea vizuri na kwamba benchi la ufundi la msimu uliopita halitavunjwa kwani ndilo lililorudisha timu hiyo Ligi Kuu na kutwaa ubingwa wa Championship.
Kuhusu usajili, Kifaru amesema wapo katika hatua za mwisho na hivi karibuni wataanza kutangaza majina ya wachezaji wapya. Aidha, amesema timu bado haijaingia kambini, lakini itaanza mazoezi ya awali muda si mrefu baada ya kumpata kocha mkuu.
Mtibwa Sugar ilishuka daraja msimu wa 2022/23, lakini imerejea Ligi Kuu baada ya kumaliza kinara kwenye Championship kwa pointi 71.